1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUjerumani

Ujerumani kupambana na uhalifu wa kupangwa

10 Agosti 2023

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani anahimiza serikali kukaza kamba dhidi ya makundi ya uhalifu uliopangwa na wanachama wa makundi hayo kufukuzwa Ujerumani, bila ya kujali iwapo wamepatikana na hatia ya uhalifu au la.

https://p.dw.com/p/4Uzkg
Deutschland Bundestag Nancy Faeser
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy FaeserPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waziri Nancy Faeser wa chama cha mrengo wa kati kushoto cha Social Democrats SPD, amegonga vichwa vya habari kwa kupendekeza sheria kali dhidi ya wanachama wa magenge ya uhalifu wanaotoka katika jamii za wahamiaji wafurushwe kutoka Ujerumani bila ya kujali iwapo watakutwa na makosa ya kuthibitisha kuhusika na uhalifu.

Pendekezo la waziri huyo wa mambo ya ndani ambalo tayari limezua ukosoaji kutoka kwa washirika wa muungano tawala- chama cha kijani, limechapishwa mapema mwezi Agosti na ni sehemu ya rasimu ya kujadiliwa bungeni.

Kwa sasa, sheria ya Ujerumani inaweka wazi kuwa wanachama wa makundi ya uhalifu uliopangwa wanaweza kufukuzwa tu ikiwa watakutwa na hatua ya uhalifu.

Soma pia: Mafunzo ya Kijerumani yatumika kama silaha ya kisiasa Poland

Sheria hiyo hata hivyo inalenga kubadilishwa na badala yake, waziri Nancy Faeser anapendekeza wahalifu kama hao kuchukuliwa kama wanachama wa makundi ya kigaidi, ambapo uanachama pekee unatosha kwa mtu kufurushwa.

Makundi ya uhalifu uliopangwa na ambao hujitambulisha kwa mizizi ya kifamilia au kikabila, huchukuliwa na polisi ya Ujerumani na katika vyombo vya habari kama "ukoo.”

Hata hivyo, wakosoaji wanasema neno "uhalifu wa ukoo” linawaweka jamaa na wanafamilia wa magenge hayo hatarini pia licha ya kutojishughulisha na uhalifu.

"Uhusiano wa familia sio kujihusisha na uhalifu,” msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani Maximilian Kall ameeleza mnamo siku ya Jumatatu baada ya pendekezo la Faeser kuibua ukosoaji mkubwa.

Kall ameongeza kuwa, kila mwanafamilia anayetishiwa kufukuzwa chini ya sheria mpya itabidi kwanza athibitishwe kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na uhalifu.

Magenge ya uhalifu wa kupangwa kufurushwa

Polisi wa Ujerumani wakifanya msako katika wilaya ya Neukoelln dhidi ya makundi ya uhalifu
Polisi wa Ujerumani wakifanya msako katika wilaya ya Neukoelln dhidi ya makundi ya uhalifuPicha: Odd Andersen/AFP

Iwapo mapendekezo hayo yataidhinishwa na kuwa sheria, inawezekana kwa watu kufurushwa iwapo kutapatikana ushahidi wa kutosha kwamba mtu ni mhalifu au ni sehemu ya makundi ya uhalifu.

Uhusiano wa mtu na makundi ya uhalifu ni lazima uchunguzwe kwanza, anasisitiza Dirk Peglow, mwenyekiti wa chama cha wafanyikazi cha BDK, ambacho kinawakilisha polisi wanaofuatilia visa vya uhalifu Ujerumani.

Peglow ameiambia DW kuwa, hio ni mojawapo ya sababu ya kuhimiza wachunguzi zaidi juu ya suala hilo badala tu ya kuwafurusha watu kiholela.

Mwenyekiti huyo wa chama cha wafanyikazi ameongeza kuwa, sio rahisi vile kufurusha watu hata iwapo mtu anayechunguzwa, ni mhalifu aliyehukumiwa.

Soma pia: Jeshi la Ujerumani linakabiliwa na ugumu wa kupata askari wapya

Suala lengine linalozua utata ni juu ya takwimu za idara ya polisi inayohusika na visa vya uhalifu unaopangwa BKA zinazoonyesha kuwa, takriban theluthi moja ya wanachama wa genge la wahalifu ni raia wa Ujerumani na hivyo basi, kuondoa uwezekano wa wahalifu hao kufurushwa.

Katika utafiti uliofanywa mwezi Januari na kundi la utafiti wa uhamiaji wa Mediendienst lenye makao yake nchini Ujerumani, mmoja wa watafiti wa kundi hilo Mahmoud Jaraba amepinga dhana iliyoenea ya kuhusisha familia nzima na uhalifu unaofanywa na mtu mmoja wa familia.

Baada ya miaka saba ya uchunguzi juu ya uhalifu uliopangwa, Jaraba ameshikilia kuwa shughuli za uhalifu hazifanywi na familia nzima na ni makosa kuibebesha lawama familia nzima kutokana na kitendo cha mtu mmoja.

Aghalabu, wanachama wengi wa familia kubwa hukosoa vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na mmoja wa jamaa zao, kwani nao pia hunyanyapaliwa au kubaguliwa na jamii kwa sababu tu wana uhusiano wa damu na wahalifu.