1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kupanguwa, kuimarisha kamandi ya jeshi

4 Aprili 2024

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, ametangaza mpango wa kupangua na kuimarisha kamandi ya jeshi la Ujerumani kama sehemu ya jitihada za kuvifanya vikosi viwe na uwezo zaidi wa ulinzi na kukabiliana na vita.

https://p.dw.com/p/4eQo7
Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, akitangaza mageuzi kwenye muundo wa jeshi la Ujerumani (Bundeswehr).Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Akizungumza mjini Berlin siku ya Alkhamis (Aprili 4) wakati wa kuwasilisha muundo mpya wa jeshi, Waziri Pistorius alisema jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) litakuwa na matawi manne ya majeshi na kamandi moja ya pamoja.

Mbali na jeshi la ardhini, jeshi la anga na jeshi la majini, tawi la nne la jeshi la Ujerumani litakuwa ni kikosi kinachohusika na mitandao, kikijikita zaidi na vita vya kielektroniki na operesheni za kwenye mtandao wa intaneti, ufuatiliaji na ulinzi wa miundombinu ya kielektroniki.

Soma zaidi: Ujerumani kuondosha wanajeshi wake Mali

Kufikia sasa, jeshi la Ujerumani limekuwa na kamandi ya kuendeshea shughuli zake kwenye mji wa Schwielowsee karibu na Potsdam kwa kupanga na kusimamia tume zake katika nchi za kigeni kama vile Afrika Magharibi na pia meli ya kivita ya Hessen katika Bahari ya Shamu.