1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kusaidia utengenezaji chanjo Afrika Kusini

31 Mei 2021

Ufaransa na Ujerumani zimeahidi kuipa Afrika Kusini msaada wa mamilioni ya Euro kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo nchini humo.

https://p.dw.com/p/3uDGT
Südafrika Bundesgesundheitsminister Jens Spahn und Adrian Kriesch Interview
Picha: DW

Akizungumza na DW akiwa mjini Pretoria, Spahn alisema Serikali ya Ujerumani imejiandaa kutoa kiasi cha hadi euro milioni 50 kwa ajili ya kuisaidia Afrika Kusini kutengeneza chanjo za corona. Amesema msaada huo unaweza kutoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya corona "Asilimia 99 ya chanjo zinazotumika hapa Afrika zinanunuliwa kutoka nje. Na tunataka kusaidia kwa sasa kutokana na hali hii ya janga. Lakini pia kwa kipindi cha katikati na cha muda mrefu, tunataka kuisaida Afrika Kusini na Afrika kwa jumla kutengeneza kiwanda chake yenyewe cha dawa kwa ajili ya utengenezaji wa chanjo."

Bundesgesundheitsminister Spahn reist nach Südafrika
Waziri Spahn akiwa na Rais wa Ufaransa Macron na mwenyeji wao RamaphosaPicha: dpa

Ujerumani inanuia kusaidia katika uhamishaji wa teknolojia, kama tu ilivyo kwa Ufaransa na Umoja wa Ulaya. Spahn amesema wanasiasa wanategemea ushirikiano wa hiari kati ya wenye hakimiliki za utengezaji chanjo, kampuni kama vile BioNTech, CureVac kutoka Ujerumani ambao wako tayari kuuwezesha mchakato huo.

Alipoulizwa kuhusu upinzani wa Ujerumani wa kuondoa hakimiliki za chanjo, Spahn alisema hakimiliki pekee haitengenezji chanjo "ushirikiano ndio njia pekee ya kufuata, Hii inahusu bidhaa ambayo ina mambo mengi. Utengenezaji wa chanjo ni mojawapo ya mambo magumu kabisa duniani. Na kwa hilo, unahitaji kwa kweli hasa kujua namna ya kutengeneza. Hakimiliki pekee haitengenezi chanjo."

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linapendekeza nchi Tajiri zitoe dozi zao za chanjo kama msaada kwa nchi maskini  badala ya kuzitumia kuwachanja watoto. Karibu mwaka mmoja uliopita, aina mpya ya kirusi cha Corona iligundulika Afrika Kusini. Tangu wakati huo Waafrika Kusini hawaruhusiwi tena kusafiri katika nchi nyingi za ulimwengu.

Wakati huo huo, waziri Spahn anakutana leo mjini Berlin na mawaziri wenzake wa afya kutoka majimbo 16 ya shirikisho la Ujerumani kujadili mifumo ya udhibiti wa vituo vya kupima virusi vya corona kufuatia tuhuma za udanganyifu. Tangu kuzuka mapema wiki hii kwa madai ya ubadhirifu katika baadhi ya vituo vya huduma hizo za upimaji, mjadala umeanza kuhusu jinsi ya kudhibiti mchakato wa upimaji na nani anayepaswa kuwa usukani. Spahn akizungumza na shirika la habari la umma ARD amesema maafisa wa afya wa serikali za mitaa wanapaswa kufuatilia vituo vya kupima corona na kukabiliana na masuala yanayohusiana na udanganyifu.

Adrian Kriesch/Bruce Amani