1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwa mwenyeji wa mkutano wa kuijadili Libya

13 Januari 2020

Ujerumani inapanga kufanya mkutano wa kilele tarehe 19 Januari, unaonuiwa kufungua njia ya amani nchini Libya.

https://p.dw.com/p/3W93p
Unionsfraktion im Bundestag, Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU)
Picha: picture-alliance/dpa/B.von Jutrczenka

Mkutano huo utakwenda sambamba na ziara ya siku moja ya rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan mjini Berlin. Ofisi ya Rais Erdogan imethibitisha bila ya kutoa maelezo mengine zaidi juu ya ziara hiyo.

Kuwepo kwa Ergogan katika mazungumzo hayo kunasemekana kuwa muhimu katika mkutano wowote wa kuijadili Libya, tangu taifa hilo lilipochukua hatua ya kupeleka washauri wake wa kijeshi Libya, jambo linaloifanya kuwa mshirika muhimu katika kutafuta amani ya vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Siku ya Jumamosi, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitangaza kufanyika kwa mkutano huo akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaongoza mazungumzo hayo iwapo mkutano utafanyika mjini Berlin. Merkel amesema pande hasimu Libya zinapaswa kuwa na jukumu kubwa iwapo suluhu itapatikana, huku akisema nia ni kuipa Libya nafasi ya kuwa nchi huru yenye amani.

Akithibitisha kufanyika kwa mkutano huo wa kilele, Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert,  amesema mkutano wa Berlin ndio mwanzo wa ufumbuzi wa mgogoro wa Libya.

Uturuki na Italia zahimiza makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano Libya

Türkei Ankara | Recep Tayyip Erdogan & Giuseppe Conte, Premierminister Italien
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Itaia Giuseppe ContePicha: picture-alliance/Anadolu Agency/H. Sagirkaya

Kwengineko Erdogan pamoja na Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte wametoa wito wa kusitishwa kabisa mapigano ya Libya kufuatia mkutano wao uliofanyika mjini Ankara.

Erdogan amesema wanatarajia makubaliano ya kusitisha mapigano yanayotarajiwa kutiwa saini hii leo yatakuwa ya kudumu.

Conte na Erdogan wamekutana wakati wakuu wa pande zinazohasimiana nchini Libya wakikutana mjini Moscow ambako wanatarajiwa kutia saini makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kabla ya mkutano wa kimataifa wa kilele unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu.

Huku hayo yakiarifiwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amekaribisha hatua ya kusitisha mapigano nchini Libya inayosimamiwa na Urusi pamoja na Uturuki lakini akaonya kuwa Umoja wa Mataifa lazima waongoze mchakato wa kuijenga  upya nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

Chanzo/Reuters/ap/afp