1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Safari za ndege zafutwa kutokana na migomo.

17 Machi 2023

Mamia ya safari za ndege kutoka na kuingia katika viwanja vinne vya ndege vya nchini Ujerumani zimekwama kutokana migomo. Hali hiyo ni sehemu ya hatua zilizoitishwa na chama cha wafanyakazi nchini Ujerumani (Verdi).

https://p.dw.com/p/4OqTA
Deutschland | Flughafen Streiks | Frankfurt am Main
Picha: Heiko Becker/REUTERS

Viwanja vinne vya ndege vya Ujerumani vimekumbwa na migomo mnamo siku ya Ijumaa, na kusababisha kuahirishwa kwa mamia ya safari za ndege. Hiyo mojawapo kati ya hatua za hivi punde zinazolenga kuvuruga utaratibu wa usafiri.

Chama cha wafanyakazi cha Ujerumani (Verdi) kimewataka wafanyakazi wa usalama na wahudumu wa ardhini katika viwanja vinne vya ndege kufanya mgomo kupinga mazingira ya kazi na malipo ya mishahara.

Abiria wamekwama kutokana na migomo ya wafanyakazi wa viwanja vya ndege.
Abiria wamekwama kutokana na migomo ya wafanyakazi wa viwanja vya ndege.Picha: AP

Migomo hiyo ni mikubwa kiasi gani?

Shirika la Viwanja vya Ndege la Ujerumani limesema migomo hiyo inatarajiwa kusababisha kuahirishwa takriban safari 681 ambapo abiria wapatao 89,000 walitarajiwa kuathirika.

Viwanja vya ndege vilivyoathiriwa ni pamoja na viwanja vilivyo na shughuli nyingi katika jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani la North Rhine-Westfalia ambavyo ni viwanja vya Düsseldorf na Cologne/Bonn Pamoja na viwanja viwili vikubwa katika jimbo la kusini la Baden-Württemberg vya Karlsruhe/Baden-Baden na Stuttgart.

Msemaji wa chama cha wafanyakazi amethibitisha migomo ya siku nzima katika viwanja  hivyo vya ndege mnamo siku ya Ijumaa ambayo imewahusisha wafanyikazi wa usalama na wahudumu wa ardhini.

Vibonzo kusisitiza malalamiko ya wafanyakazi wanaodai nyongeza ya mishahara.
Vibonzo kusisitiza malalamiko ya wafanyakazi wanaodai nyongeza ya mishahara.Picha: dpa

Mjini Cologne, karibu safari za ndege 144 kati ya safari 148 zilizopangwa awali Pamoja na kutua kwa ndege za abiria - hazikufanyika, kwa mujibu wa msemaji huyo wa Verdi. Huko mjini Düsseldorf wafanyikazi 500 waligoma huku safri zipatazo 264 kati ya safari 391 ziliathiriwa.

Mfululizo wa migomo katika sekta ya usafiri

Mapema wiki, kulikuwa na mgomo katika viwanja vya ndege katika miji ya Berlin, Bremen, na Hamburg wakati ambapo safari za ndege zimeathirika kutokana na janga la corona lililosababisha kuwepo na uhaba wa wafanyikazi jambo ambalo wachache waliopo wanadai nyongeza ya mishahara. Chama cha wafanyakazi nchini Ujerumani (Verdi) kimeitisha migomo baada ya mazungumzo kushindwa fanikiwa kati ya sekta ya viwanda na wakuu wa sekta ya umma katika sekta nyinginezo mbalimbali, hasa katika maeneo ya usafiri na afya.

Kampuni ya uchukuzi wa umma ya mji wa magharibi mwa Ujerumaji wa Cologne imesema inatarajia usafiri katika eneo hilo utakabiliwa na mgomo mwingine siku za Jumatatu na Jumanne wiki ijayo. Mazungumzo yanaendelea yanayowawakilisha takriban wafanyakazi milioni 2.5 wa taifa na wa manispaa kote nchini ambao wanadai nyongeza ya mishahara ya asilimia 10.5, au angalau kiasi cha Euro 500 zaidi kwa mwezi.

Onyo juu ya kutokea migomo zaidi kwenye sekta ya usafirishaji
Onyo juu ya kutokea migomo zaidi kwenye sekta ya usafirishajiPicha: AP

Kufikia sasa, waajiri wametoa tu nyongeza ya asilimia 5 katika hatua mbili na malipo ya mara moja ya Euro 2,500 huku duru ya tatu ya mazungumzo imepangiwa kufanyika tarehe 27 hadi tarehe 29 mwezi Machi. Chama cha wafanyakazi nchini Ujerumani (Verdi) kimesema pia kimeitisha mgomo wa kitaifa kwa wafanyakazi wa hospitali, kliniki za wagonjwa wa akili, nyumba za wazee na huduma za dharura.

Kulikuwa na migomo katika hospitali kadhaa katika miji ya kaskazini ya Hamburg na Kiel mnamo siku ya Jumatano, na katika maeneo mengine ya nchi, pamoja na kwenye baadhi ya vituo vya kuwatunza watoto mchana, maarufu - Day Care.

Chanzo: DPA/DW