Scholz: Tutaendelea kuiunga mkono Ukraine kwa muda wote
14 Mei 2024Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Sweden, Denmark, Finland, Iceland na Norway mjini Stockholm amesema, nchi hizo zitaendelea kuiunga mkono kwa dhati Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Finland Petteri Orpo ameeleza kuwa hali katika uwanja wa vita mkoani Kharkiv sio ya kuridhisha na kusisitiza hatua za haraka kuchukuliwa na mataifa ya Magharibi ili kuzuia hali kama ilivyotokea Mariupol.
Soma pia: Wanachama wa NATO watakiwa kuitikia wito wa Ukraine
Mariupol ni mji wa bandari unaokaliwa na Urusi kusini mashariki mwa Ukraine na ambao uliharibiwa na kutekwa katika miezi ya kwanza ya vita mnamo mwaka 2022.
Licha ya majadiliano hayo mjini Stockholm, hakuna ahadi mpya kama vile mfumo wa ulinzi wa anga aina ya Patriot, zilizotangazwa.
Scholz anatarajiwa kuendelea na ziara yake nchini Sweden leo na baadaye atakutana na Waziri Mkuu Ulf Kristersson kwa mazungumzo.