1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na washirika wake wamshinikiza Nicolas Maduro

26 Januari 2019

Nchi tatu za Ulaya Ujerumani, Ufaransa na Uhispania zimemtaka rais wa Venezuela Nicolas Maduro kuitisha uchaguzi mpya la sivyo nchi hizo pia zitamtambua kiongozi wa upinzani Juan Guiado kama rais.

https://p.dw.com/p/3CFWO
Kombibild Venezuela Maduro und Guaido
Picha: Getty Images/AFP/Y. Cortez/F. Parra

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ambaye urais wake unakabiliwa na utata amepewa siku nane kutangaza uchaguzi mpya nchini mwake. Nchi zilizotoa agizo hilo ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Uhispania ambazo zimesema iwapo Maduro hatatoa tangazo hilo kwa kipindi hicho basi watamtambua kiongozi wa upinzani kama rais wa Venezuela.

Naibu msemaji wa serikali ya Ujerumani Martina Fietz ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba raia wa Venezuela wanastahili kuamua kuhusu mustakabali wa nchi yao kwa uhuru na usalama. Baada ya kujitangaza kama rais wa muda, Guaido aliungwa mkono na mataifa kadhaa duniani ikiwemo Marekani.

Agizo hilo ni la wazi kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wakati ambapo nchi hizo wanachama 28 bado zinapanga kutoa taarifa ya pamoja kuhusiana na msimamo wake juu ya mgogoro wa Venezuela. Mnamo siku ya Ijumaa Ujerumani na Uhispania zilizoa mwito wa kufanyika uchaguzi mpya nchini Venezuela lakini bila kutoa muda wa mwisho wa agizo hilo.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Reuters/M. Quintero

Maduro, aliingia mamlakani mwaka 2013 baada ya kumrithi aliyekua kiongozi maarufu wa nchi hiyo marehemu Hugo Chavez. Rais huyo wa Venezuela ameshuhudia nchi yake ikitumbukia katika mgogoro tangu uchumi wake kupungua kutokana na bei ya mafuta ya kuanguka. Sera za kijamii zilizoanzishwa na mtangulizi wake, zimekuwa mzigo wa kiuchumi ambao umesababisha kupanda gharama za maisha, ukosefu mkubwa wa ajira na uhaba wa bidhaa za msingi.

Maduro alishinda muhula wa pili mnamo mwezi Mei mwaka uliopita katika kura ambayo upinzani na baadhi ya nchi jirani zinasema ulikua wa udanganyifu, hali ambayo imesababisha shinikizo la kumtaka rais huyo ajiuzulu. Hadi sasa, Maduro bado anadhibiti uaminifu wa jeshi la nchi hiyo lenye nguvu.

Nchi kadhaa za ulimwengu zimejitosa kwenye mgogoro wa Venezuela inachukua pande juu ya mapambano ya nguvu nchini Venezuela. Juan Guaido mwenye umri wa miaka 35 ambaye pia ni spika wa Bunge, wiki hii alijitangaza mwenyewe kuwa rais.

Marekani, Brazili, Argentina na nchi nyingine tayari zimemuunga mkono Guaido na kumkataa Maduro. Tangu ajitangaze kuwa kiongozi wa mpito, Guaido amekataa kufanya mazungumzo na Maduro na badala yake ameitisha maandamano makubwa zaidi

Mwandishi:Zainab Aziz/ p.dw.com/p/3CF9k

Mhariri: Jacob Safari