Ujerumani, Ufaransa kushirikiana mpango wa ndege za kivita
26 Aprili 2018Hatua hii itaanzisha mradi uliozinduliwa kwa mara ya kwanza Julai mwaka jana na maafisa kutoka mataifa yote mawili watasaini waraka wa uainishaji kandoni mwa maonyesho ya ndege za kivita ya Berlin ILA, yaliofunguliwa na kansela Angelea Merkel siku ya Jumatano.
Pamoja na kuwa na uwezo wa kufanyakazi kivyake, au kuongoza kundi lingine la ndege zikiwemo zisizo na rubani, ndege hiyo itahitaji pia kuwa na uwezo wa kuendesha operesheni za mashambulizi na kujihami, walisema maafisa wa wizara ya ulinzi ya Ujerumani.
Ilikuwa haijaamuliwa bado iwapo ndege hiyo mpya itakuwa inaendeshwa tu na rubani au itakuwa pia na toleo la isiyokuwa na rubani. Lengo ni kuanza kuzitumia ndege hizo mpya, zikiwa na uwezo wenye mipaka, kuanzia mwaka 2040.
Juhudi za kuondoa ushindani wa miradi sawa
Hatua ya kutengeneza ndege mpya inaonekana kama ya mwanzo kuelekea kuondoa tofauti zilizoiacha Ulaya ikipambana kuendeleza miradi mitatu yenye kushindana - mradi wa Rafale wa Ufaransa, Eurofighter - unaoziwakilisha Ujerumani, Uingereza, Italia na Uhispania - na ule wa Gripen wa Sweden.
Merkel na Emmanuel Macron walizindua mipango ya programu mpya muda mfupi baada ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa mwezi Mei katika ishara muhimu iliosanifiwa kutoa motisha mpya kwa uhusiano kati ya Ufaransa na Ujerumani baada ya Uingereza kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Wataalamu wengi wa ulinzi wanaamini Uingereza hatimaye itaalikwa tena kujiunga na programu hiyo.
Tamko la nia ya kisiasa linatarajiwa kufuatiwa na tangazo la kisekta linalotoa ufafanuzi namna washirika, hususani mashirika ya usafiri wa anga ya Dassault na Airbus, makampuni ya ulinzi ya Ujerumani ya aeronautics champion na Eurofighter, yatakavyouendea mradi huo mkubwa wa mabilioni ya dola.
Awali Ufaransa ilikuwa sehemu ya ubia unaozihusisha Uingereza, Ujerumani na Italia, lakini iliamua katika miaka ya 1980 kuanzisha ndege yake ya kivita ya Rafale inayotengenezwa na kampuni ya Dassault, kwa sehemu ili kuhakikisha thamani ya juu ya kazi ya shirika lake hilo la utenegezaji injini, ambalo sasa ni sehemu ya Safran.
Airbus na Dassault yalikataa kutoa tamko lolote kabla ya maonyesho ya ILA ya Berlin.
Ushirikian zaidi kati ya Ufaransa na Ujerumani
Ujerumani na Ufaransa pia zinapanga kusiani waraka katika maonyesho hayo kuangalia uwezekano wa kutengeneza kwa pamoja, ndege mpya ya uchunguzi wa baharini, zikiwa na lengo kuanza kuitumia ifikapo 2035, duru kutoka jeshi la Ujerumani zilisema.
Waziri wa ulinzi wa Ujeurmani Ursula von der Leyen atajadili njia ya kuimarisha mifumo ya ulinzi ya Ulaya na NATO akiwa pamoja na mwenzake wa Ufaransa, Florence Parly, ambaye yuko ziarani mjini Berlin.
Ufaransa na Ujerumani tayari zinashirikiana katika operesheni kadhaa na miradi, ikiwemo kutuma vikosi nchini Mali na mpango wa kupata na kisha kuendesha kwa pamoja, kundi la ndege za usafirishaji aina ya C-130J zilizotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin ya Marekani.
Mwandishi. Iddi Ssessanga/rtrr
Mhariri: Josephat Charo