1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa makubwa ya Ulaya yataka mapigano yasitishwe Gaza

12 Agosti 2024

Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wameunga mkono miito ya kusitishwa mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, kurejeshwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/4jNLq
Mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza
Vikosi vya Israel vimeendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa GazaPicha: Omar Al-Qattaa/AFP/Getty Images

Katika tamko la pamoja walilolitoa leo Jumatatu, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer, wamesema wanaunga mkono kikamilifu jitihada za hivi karibuni za Marekani, Qatar na Misri ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita vilivyodumu kwa kipindi cha miezi 10.

Soma pia: Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zasema vita vya Gaza viishe

Mataifa hayo matatu yaliyojipa jukumu la upatanishi yamekuwa yakijaribu kuzishawishi pande hasimu zikubali mpango wa awamu tatu wa kusitisha vita uliopendekezwa na Rais Joe Biden wa Marekani.

Mbali ya suala la Gaza, tamko la Scholz, Macron na Starmer limeirai pia Iran na washirika wake kujizuia dhidi ya hatua zozote za kijeshi ambazo zitachochea mivutano kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.