Ujerumani yaadhimisha miaka 30 ya kuanguka Ukuta wa Berlin
10 Novemba 2019Ujerumani imeadhimisha miaka 30 ya kuangushwa kwa Ukuta wa Berlin, tukio muhimu katika kuanguka kwa enzio ya ukomunisti katika mashariki ya Ulaya. Kansela Angela Merkel na Rais Frank-Walter Steinmeier waliongoza sherehe rasmi, ambazo zilifanyika katika lango la kihistoria la Brandenburg na Mtaa wa Bernauer ambako sehemu za mwisho za ukuta huo zinapatikana.
Kwingineko mjini Berlin, kulikuwa na matamasha ya muziki, midahalo ya umma likiwemo tamasha la muziki katika Lango la Brandenburg.
Merkel: 'Ukuta wa Berlin ni historia'
Merkel alizungumza katika Kanisa la Maridhiano, ambalo lilijengwa katika sehemu ambayo utawala wa Ujerumani ya Mashariki ulibomoa kanisa ili kuwapa walenga shabaha nafasi nzuri ya kuwaona watu wanaokimbilia Magharibi.
"Nakumbuka wale waliouawa kwenye ukuta huu kwa sababu walikuwa wakitadfuta uhuru," alisema Merkel katika hafla hiyo ya kumbukumbu. "Tunataka kuhakikisha kuwa hakuna ukuta utakaowatenganisha watu tena," alisema.
"Ukuta wa Berlin ni historia. Inayotufunza hiki: Hakuna ukuta unaowatenganisha watu na kudhibiti uhuru ni mrefu Zaidi au mpana Zaidi kiasi kwamba hauwezi kupitika.”
Katika sherehe zilizofanywa kwenye Lango la Brandenburg, Steinmeier aligusia pengo kubwa ambalo bado lipo kati ya mashariki na magharibi, ambalo limeongezeka huku wimbi la siasa kali za mrengo wa kulia likisambaa katika iliyokuwa mashariki ya kikomunisti.
"Ukuta mpya umejengwa ambao unapita katikati ya nchi yetu – ukuta wa kukatisha tamaa, ukuta wa hasira na chuki,” alisema Steinmeier.
"Kuta zisizoonekana lakini zinazotenganisha. Kuta zinazosimama mbele ya mshikamano,” alionya, wakati akiwataka Wajerumani "kuziporomosha kuta hizi, mwishowe."
"Jioni hii, tunasimama hapa tukiwa wenye shukrani, hata tukiwa na machozi machoni mwetu."
Hisia kutoka kote duniani
Kumbukumbu na hisia tofauti ziliendelea kumiminika kutoka kote duniani. Rais anayeondoka wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker alielezea tukio la kuangushwa Ukuta wa Berlin kuwa ni "mapinduzi ya amani," yaliyoongozwa na watu "waliojitolea uhuru wao kwa ajili ya kupata uhuru wa kila mmoja."
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia aliwasifu watu waliopambana hadi mwisho ili kufanikisha muungano wa Ujerumani.
"Ukuta wa Berlin haukuanguka miaka 30 iliyopita," amesema Macron katika ujumbe wa Twitter ulioandikwa kwenye Kifaransa na Kijerumani. "uliangushwa na ujasiri wa maelfu ya watu waliotamani uhuru, na kutoa nafasi ya kuunganishwa Ujerumani na umoja wa Ulaya. Pia nasi tuwe na ujasiri na kuyatimiza matarajio yao."