Ujerumani yaadhimisha miaka 33 ya kuungana tena
4 Oktoba 2023Oktoba 3 mwaka 1990 ilikuwa siku ya kihistoria kwa Ujerumani pale pande mbili za taifa hilo zilipoungana tena baada ya kutengana kwa zaidi ya miaka 40.
Tukio hilo la muungano lilikuwa ni matokeo ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin, alama kuu ya utengano kati ya iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani Mashariki (GDR) na ile ya upande wa magharibi.
Kulikuwa na shamra shamra miaka 33 iliyopita pale pande hizo mbili zilizotenganishwa siyo tu kwa ukuta bali hata mitazamo ya kisiasa na njia za uendeshaji uchumi zilipojiunga tena kuunda taifa moja la shirikisho la Ujerumani.
Tangu wakati huo hadi hii leo Oktoba tatu ni siku ya kitaifa na ya mapumziko nchini Ujerumani ikiambatana na matukio mbalimbali ya kuadhimisha siku minyororo ya utengano ilipokatika.
Kansela Scholz na Rais Steinmeier watoa mwito wa kuenziwa demokrasia na amani
Hii leo sherehe za maadhimisho hayo zinafanyika huko Hamburg, mji wenye hadhi ya jimbo ambao kwa sasa ndiyo unashikilia urais wa zamu wa Baraza la Juu la Bunge la Ujerumani, Bundesrat.
Hafla rasmi ya kitaifa inafanyika katika mji mdogo wa bandari huko kaskazini mwa Hamburg wa Elbphilharmonie na itajumuisha hotuba kutoka mkuu wa mahakama ya katiba nchini Ujerumani Stephan Harbarth.
Zaidi ya watu 1,300 ikiwemo viongozi wa kitaifa na wakuu wa serikali 16 za majimbo ya Ujerumani wamealikwa kuhudhuria.
Katika ujumbe wake kwa siku ya muungano kansela Olaf Scholz amesema tarehe 03 Oktoba inawakumbusha wajerumani kuwa amani, uhuru na demokrasia siyo vitu vitolewavywe kwenye sahani ya shaba bali ni misingi inayopaswa kulindwa kwa kila raia kusimama imara na kuitetea.
Ujumbe sawa na huo umetolewa pia na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steimeier kwenye mahojiano aliyoyafanya jana usiku na kituo cha televisheni cha Ujerumani cha ARD.
Nini kilitokea baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia?
Yafaa kukumbusha kuwa historia mashaka ya utengano yalizuka wiki kadhaa tu baada ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya duniani mnamo mwaka 1945.
Ujerumani iliyokuwa miongoni mwa madola makubwa yaliyopigana vita hivyo ilipoteza mbele kundi la mataifa manne washirika yaani Uingereza, Marekani, Ufaransa na uliokuwa Muungano wa Kisovieti.
Madola hayo yalifikia makubaliano ya kuiagawa nchi hiyo ili kuivunja nguvu ya kurejea kwa uchokozi siku za usoni.
Taifa hilo likagawanywa vipande vinne na vile vitatu vya Marekani, Uingereza na Ufaransa viliungana kwa jina la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani liliofuata siasa ya demokrasia ya vyama vingi na uchumi wa kibepari.
Kanda la Kirusi ikaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani iliyofuata siasa ya utawala wa chama cha kikomunisti na uchumi wa kijamaa.
Miaka 33 ya mafanikio na msukuko kati ya pande mbili ziliungana tena
Katika maadhimisho ya miaka 33 ya mwaka huu kumechapishwa ripoti inayoonesha kuwa bado migawanyiko ingalimo ndani ya Ujerumani mpya
Ripoti hiyo inasema miongoni mwa mafanikio ya kiuchumi ni viwango vya pensheni kuwekwa sawa kwa nchi nzima kuanzia mwaka huu wa 2023, lakini hili limekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu ya Wajerumani waliokuwa wakiishi kwenye upande wa mashariki.
Hata hivyo, bado kuna pengo kubwa kwenye viwango vya mishahara na utajiri baina ya pande hizi mbili.
Hii ni hata baada ya kutegemewa kuwa uchumi wa mashariki ungelikuja juu sana kutokana na kuwa kwake kitovu cha uwekezaji wa viwanda vya ngazi ya kati.