Ujerumani yaadhimisha miaka 500 ya mabadiliko
31 Oktoba 2017Ni katika mji huo ambapo kasisi wa Kijerumani Martin Luther aliongoza mgawanyiko katika Kanisa Katoliki katika mojawapo ya matukio muhimu zaidi barani Ulaya.
Akiwa profesa wa thiolojia na kasisi, Luther alipinga mamlaka ya Vatican na alitilia shaka mafundisho ya Kanisa Katoliki na yaliyofanywa na Kanisa hilo kupitia ile michanganuo yake maarufu 95. Anaaminika kuwa aliibandika michanganuo hiyo katika mlango wa kanisa la Wittenberg mnamo Oktoba 31 mwaka 1517.
Kama kumbukumbu nyengine zote za Luther katika jimbo la Saxony-Anhalt mashariki mwa Ujerumani, mlango wa kanisa hilo umeorodheshwa kama kumbukumbu muhimu na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO.
Viongozi mashuhuru wanatarajiwa kuhudhuria
Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier, Kansela Angela Merkel na Mkuu wa jimbo la wa Saxony-Anhalt Reiner Haseloff pamoja na wageni wengine wengi mashuhuri kutoka Ujerumani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo.
Kansela Merkel amesema sherehe hii ambayo ni siku ya ya kitaifa Ujerumani, inatoa nafasi ya kutafakari mageuzi yaliyotokana na mabadiliko hayo yaliyoletwa na Martin Luther.
Wanamziki pamoja na wachekeshaji ni miongoni mwa watu wanaotarajiwa kuwepo katika sherehe hizo katika harakati za kuzifufua fikra za enzi ambazo Martin Luther alikuwa akiishi bado.
Zaidi ya hayo, kuna mpango wa maonesho ya sanaa pamoja na tamasha la mataa na katika sehemu zengine za nchi, msururu wa mambo ya kuadhimisha mabadiliko aliyoyaleta Luther yanaendelea.
Huku hayo yakiarifiwa zaidi ya watu 600 katika mji wa Kusini Magharibi wa Mannheim, waliandika kwa mkono tafsiri ya Biblia, kama mojawapo ya njia za kusherehekea maadhimisho ya miaka 500 ya mabadiliko.
Huko Mannheim watu wanafanya tafsiri ya Biblia kuadhimisha siku hii
Kasisi Stefan Scholpp kutoka kanisa la Kiinjili katika eneo hilo anasema, "washiriki walikuwa kati ya umri wa miaka 8 hadi 99 na wanawakilisha watu wengi wa matabaka mbali mbali," alisema Scholpp, "kutoka kanisa la Kiinjili la Ujerumani, mwenyekiti wa baraza Heinrich Bedform-Strohm, hadi mfungwa aliye katika gereza la Mannheim," aliongeza Kasisi huyo.
Baada ya kufanya tafsiri, kulikuwa na wahariri waliokuwa wanapitia kile kilichoandikwa na washirika katika mradi huo wa kuitafsiri Biblia, na Scholpp amesema walilazimika kusahihisha makosa kadhaa ingawa hakuna wakati wowote ambapo walikumbana na kisa ambapo kulikuwa na mtu aliyekufuru katika kutafsiri.
Yatakayotokana na mradi huo ulioanza mwezi Aprili, yatajumuishwa katika kitabu kikuu kitakachokuwa na kurasa 3,626 na Scholpp anapanga kuitumia Biblia hiyo kama Biblia ya altare katika kanisa lake huko Mannheim.
Mwandishi: Jacob Safari/DPAE
Mhariri: Gakuba Daniel