Ujerumani yaanzisha sherehe za miaka 30 ya muungano
5 Septemba 2020Bila shaka, badala ya kuadhimisha muungano hapo Oktoba 3, siku inayofahamika kama Siku ya Umoja, mlolongo wa matukio madogo madogo yanapangwa katika mwezi mzima, kuepusha mikusanyiko mikubwa na kupunguza kitisho cha kusambaa kwa COVID-19.
Potsdam , mji mkuu wa jimbo la mashariki mwa Ujerumani la Brandenburg, utakuwa ukiangiliwa kwa karibu katika sherehe hizi za mwaka 2020.
Matukio ya mwaka huu ya muungano pia yanakuja chini ya mwaka mmoja baada ya Ujerumani kuadhimisha miaka 30 ya kuvunjika kwa ukuta wa Berlin, ikiwa ndio wakati muhimu katika historia ya taifa hilo ambao ulisafisha njia katika kufikisha mwisho mgawanyiko uliotokea nchini humo katika wakati wa vita baridi.
Lakini badala ya kuneemeka kwa hali ya nchi kama ilivyoahidiwa na kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl kufuatia kuanguka kwa ukuta, muungano umethibitisha kuwa ni mradi ghali na wenye utata kwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika bara la Ulaya.
Muungano wa Ujerumani
Bado kuna uungwaji mkono mkubwa katika taifa hilo kwa ajili ya muungano, ambao umeweka kando zaidi ya miaka 40 ya ukomunist katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo na kusaidia Ujerumani kuchukua jukumu la mbele katika medani ya kimataifa.
Hata hivyo , miaka 30 baada ya oande mbili za Ujerumani kuungana tena, tofauti kubwa za kijamii na kiuchumi zinaendelea kuwapo kati ya maeneo ya nchi hiyo ya mashariki na magharibi.
Taifa hilo pia linapambana na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na kuna hofu kuwa sherehe za muungano zinaweza zikachafuliwa na makabiliano kati ya makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia pamoja na watu wanaofanya maandamano ya kupinga hatua zinazochukuliwa kudhibiti virusi vya corona pamoja na waandamanaji wanaopinga makundi hayo.