Ujerumani yaibamiza Scotland 5-1 ufunguzi michuano ya EURO
15 Juni 2024Ulikuwa mchezo uliowaacha Wajerumani meno yote nje kwa bashasha na kuibua matumaini ya taifa zima kwamba timu yao ´Die Mannschaft´ inaweza kuwatoa kimasomaso katika michuano hiyo iliyoanza usiku wa kuamkia leo mjini Munich.
Goli la dakika za mwanzo mwanzo la Florian Wirtz na lile la katikati mwa kipindi cha kwanza liliofungwa na Jamal Musiala yalitoa ishara za mapema kabisa kwamba timu hiyo mwenyeji ingekuwa na mwanzo mzuri.
"Hakika hii ndiyo namna tuliyotaka kufungua michuano hii na kusema kweli tulihitaji mwanzo wa aina hiyo," amekaririwa nahodha wa kikosi cha Ujerumani Ilkay Gündogan alipozungumza na Kituo cha Utangazaji cha Taifa, ZDF.
Matarajio ya kabla ya michuano hii miongoni mwa Wajerumani yalikuwa madogo ikitiliwa maanani kwamba timu yao ya taifa ilivurunda vibaya sana katika mashindano matatu ya mwisho ya kandanda.
Lakini kwa mchezo waliouonesha usiku wa kuamkia leo vijana wa kocha Julian Nagelsmann wamefufua matumaini ya taifa zima kwamba huenda wanaweza kuja kucheza fainaliza Euro wiki nne zinazokuja mjini Berlin.
Vijana wa Nagelsmann watawala mchezo na kuiendesha Scotland msobemsobe
Kikosi cha Ujerumani kilitawala mchezo dakika zote 45 za mwanzo na maji yalizidi unga kwa upande wa Scotland baada ya mlinzi wake Ryan Porteous kuambulia kadi nyekundu kwa kufanya madhambi kwenye eneo la 18.
Baada ya adhabu mwamuzi aliipatia pia Ujerumani mkwaju wa penalti uliotiwa wavuni na Kai Havertz. Hadi kipyenga kinapulizwa kwenda mapumziko Ujerumani ilikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Mabadiliko yaliyofanywa na kikosi cha Ujerumani mnamo kipindi cha pili yalisadifu kuwa mwiba mchungu kwa Scotland.
Vijana machachari Niclas Füllkrug na Emre Can wote wakitokea benchi walifanya maajabu kwa kupachika mabao mawili. La Füllkrug ilikuwa dakika 68 na lile la Can mnamo dakika tatu za nyongeza kabla ya firimbi ya mwisho kupulizwa.
"Dakika 20 za kwanza zilikuwa za kusisimua. Magoli ya mwanzo yalikuwa mazuri na ni muhimu sana kwamba wachezaji wote walionesha mchezo wa kuvutia," amesema Julian Nagelsmann, kocha wa Die Mannschaft muda mfupi baada ya mechi kumalizika.
Scotland itamudu kufurukuta ili kusonga mbele kutokea kundi A?
Scotland ambao hawakuwafanikiwa hata kulisogelea lango la Ujerumani, waliishia kuwapa furaha mashabiki wako kwa goli moja la mlinzi wa Ujerumani Antonio Rüdiger kujifunga mwenyewe mnamo dakika ya 87.
Inaonesha wazi kwamba kocha wa Scotland Steve Clarke itafaa ajipange upya atakapokutana na Hungray na baadaye Uswisi ikiwa anataka timu yake isonge mbele kutoka kundi A.
"Ulikuwa usiku mgumu. Hatukucheza kwa kiwango chetu. Timu ya Ujerumani ilikuwa madhubuti," amesema Clarke alipozungumza na waandishi habari baada ya mchezo.
Baadaye leo jioni kutakuwa na mchezo wa pili wa kundi A. Hungary itakuwa na miada na Uswisi.
Katika mechi mbili za kundi B zitakazopigwa pia leo Uhispania inaingojea Croatia wakati Albania itawatunishia misuli Italia ambao ni mabingwa watetezi wa kombe la Euro.