1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ujerumani yaishukuru Ufaransa kwa kuwaondoa raia wake Niger

1 Agosti 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameishukuru Ufaransa kwa kusaidia kuwaondoa raia wake Niger, ambako mapinduzi ya kijeshi yalifanyika wiki iliyopita na kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.

https://p.dw.com/p/4UeeB
Frankreich Paris | Treffen zur Situation im Niger
Maafisa wa Ufaransa wakijadiliana kuhusu kinachoendelea NigerPicha: Stefano Rellandini/AFP/Getty Images

Katika taarifa yake aliyoitoa Jumanne, Baerbock amesema kipaumbele cha kwanza kwa Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani kwa wakati huu, bila shaka ni usalama wa raia wa Ujerumani walioko Niger.

Amesema kama ilivyokuwa kwa mizozo iliyopita, wanashirikiana kwa karibu na Ufaransa na washirika wengine wa Ulaya katika kulishughulikia hilo.

Raia washauriwa kuondoka Niamey

Mapema wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani iliwashauri raia wake kuondoka Niamey kwa kutumia ndege maalum zilizotolewa na Ufaransa, ambayo awali ilitangaza itaanza Jumanne kuwaondoa nchini humo raia wake na wa Umoja wa Ulaya kwa ujumla.

Wizara hiyo imesema wamethibitisha kuwa wenzao wa Ufaransa wamejitolea kuwachukua raia wa Ujerumani kwenye ndege zao, na hivyo kuwataka Wajerumani kuukubali msaada huo.

Deutsche Außenministerin Annalena Baerbock im Gespräch mit DW
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: DW

Ujerumani imesema inakadiria kuwa chini ya raia 100 wako Niger kwa sasa, ukiwaondoa maafisa walioko nchini humo kama sehemu ya ujumbe wa kijeshi wa Ujerumani.

Uhispania nayo imetangaza leo kuwa itawaondoa raia wake zaidi ya 70 Niger kwa kutumia usafiri wa anga. Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Uhispania haijaeleza wazi iwapo itawaondoa raia wake kwa kutumia ndege zake yenyewe, kutokana na sababu za kiusalama.

Leo asubuhi Italia nayo ilitangaza kupeleka ndege maalum kwa ajili ya kuwaondoa raia wake Niger.

Ulaya yataka Bazoum aachiwe huru

Wakati huo huo, Msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Nabila Massrali leo ametoa wito wa kuachiwa huru kwa Rais Bazoum, akisema umoja huo unalaani vikali mapinduzi ya kijeshi.

"Msimamo wetu kisiasa uko wazi kabisa. Tunalaani vikali mapinduzi haya, ambayo kwetu ni kitisho cha demokrasia na utulivu wa Niger. Tunatoa wito wa kuachiwa mara moja Rais Bazoum, familia yake na wasaidizi wake," alifafanua Nabila.

Coup aftermath in Niger
Maafisa wa jeshi waliohusika na mapinduzi NigerPicha: Balima Boureima/REUTERS

Nabila amesema wanaunga mkono kwa dhati hatua iliyochukuliwa na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, ya kuweka vikwazo vya kichumi na usafiri dhidi ya wanajeshi waliohusika na mapinduzi.

Mapinduzi kutoathiri usambazaji wa urani

Niger pia ni msafirishaji wa madini ya urani, lakini Umoja wa Ulaya umesema hakuna hatari ya usambazaji wa madini hayo kutokana na mapinduzi ya kijeshi.

Umoja huo umesema madini mengi asilia kutoka Niger yanayopelekwa Ulaya, yanarutubishwa Ufaransa na kisha kuna sehemu ambayo inarutubishwa Uhispania, hivyo kuna akiba ya kutosha kwenye soko la dunia ili kukidhi mahitaji ya Umoja wa Ulaya.

(AFP, AP, DPA, Reuters)