1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaitisha ukanda wa usalama Syria

22 Oktoba 2019

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer amependekeza kuundwa ukanda wa kimataifa wa usalama Syria. Amesema ataujadili mpango huo pembezoni mwa mkutano wa NATO mjini Brussels Alhamis na Ijumaa wiki hii. 

https://p.dw.com/p/3Rgnh
Syrien Türkische Soldaten in Tal Abyad
Picha: picture-alliance/Xinhua

Katika mahojiano na DW, Annegret Kramp-Karenbauer amesema kuwa mpango huo uliratibiwa na Kansela Angela Merkel na kuwasilishwa kwa washirika wa nchi za Magharibi. Waziri huyo wa ulinzi ambaye pia ni kiongozi wa chama cha  Christian Democratic Union - CDU amesema ukanda huo unaweza kusimamiwa kwa ushirikiano na Uturuki na Urusi.

"Ukanda huo wa usalama utaanzisha upya vita dhidi ya ugaidi na dhidi ya Dola la Kiislamu - IS ambavyo kwa sasa vimesimama. Aidha utasaidia kurejesha utulivu wa kikanda ili iwe rahisi kuanza kuyajenga upya maisha ya raia ili wale waliokimbia waweze kurejea makwao kwa hiari" Amesema AKK

Pendekezo lolote hata hivyo lazima kwanza liidhinishwe na baraza la mawaziri la Ujerumani na bunge lake – Bundestag. Lakini Waziri Kramp-Karrenbauer amesema Ulaya haipaswi kuwa mtazamaji tu katika suala hilo, akiongeza kuwa lazima watayarishe mapendekezo yao wenyewe na kuanzisha mazungumzo.

Bundestag - Fortsetzung Haushaltswoche
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani AKKPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Wiki iliyopita Kansela Merkel alipendekeza kuandaliwa mkutano wa kilele na Ufaransa, Uingereza na Uturuki ili kujadili hali inayoendelea kuwa mbaya kaskazini mwa Syria. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kiutu inasema kiasi ya raia 160,000 wameachwa bila makaazi tangu kuanza kwa operesheni ya Uturuki mnamo Oktoba 9.

Sasa, waziri Kramp-Karrenbauer anatoa wito wa mapendekezo madhubuti ya kuundwa eneo salama yajadiliwe katika Muungano wa muda mrefu wa Ulinzi na Usalama kati ya Ufaransa na Uingereza, pamoja na Uingereza. Amesema lazima Uturuki na Urusi zishirikishwe katika mpango huo.

Hayo yakijiri, Rais wa Urusi Vladmir Putin anatarajiwa kumualika leo mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kwa  mazungumzo kuhusu mustakabali wa mzozo wa Syria, wakati muda wa mpango wa kusitisha mapigano uliosimamiwa na Marekani unatarajiwa kumalizika.

Mpango huo wa kuweka chini silaha kwa saa 120 unatarajiwa kufikia tamati leo usiku. Taarifa ya Ikulu ya Urusi inasema mazungumzo ya Putin na Erdogan yatalenga katika kurejesha hali ya kawaida kaskazini mwa Syria. Mazungumzo hayo yanaripotiwa kupangwa kufanyika katika mji wa kusini mwa Urusi wa Sochi.