1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yajizatiti kuisaidia zaidi Ukraine

14 Februari 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema leo kwamba anaangazia kuendelea kupeleka misaada nchini Ukraine, katikati ya mvutano unaozidi kuongezeka na Urusi. Kansela Scholz amesema hayo akiwa ziarani nchini Ukraine. 

https://p.dw.com/p/470CF
Ukraine | PK Selenskyj und Scholz in Kiew
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Olaf Scholz amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwamba hakuna taifa ulimwenguni ambalo limetoa msaada mkubwa wa kiuchumi katika miaka minane iliyopita nchini Ukraine zaidi ya Ujerumani ambayo iliipatia zaidi ya dola bilioni 2 za msaada.

Amesema imeisaidia Kyiv kujisimamia yenyewe dhidi ya ushawishi wowote wa kigeni na kuongeza kuwa wamejizatiti kuendeleza msaada huo.

Kansela Scholz aidha amesema anatarajia Urusi itaanzisha hatua za wazi za kupunguza mvutano na Ukraine na kuongeza kuwa Ujerumani na washirika wake wa magharibi tayari wamejiandaa na mazungumzo magumu na Urusi kuhusiana na usalama wa Ulaya.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemwambia kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwamba Urusi ilikuwa ikitumia bomba lake la gesi la Nord Stream 2 kama "silaha dhidi ya mfumo wa siasa za kimaeneo".

Nord Stream 2 Ostseepipeline
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky asisitiza kwamba mradi wa Urusi na Ujerumani wa Nord Stream 2 unatumiwa na Urusi kama silaha dhidi yake.Picha: Stefan Sauer/dpa/picture alliance

Amesema baada ya mazungumzo na kansela Scholz mjini Kyiv kwamba kuna tofauti baina yao katika tathmini juu ya uhusiano wa masuala ya nishati uliopo kati ya Urusi na Ujerumani na kusisitiza kuwa wanatambua wazi kuwa hiyo ni silaha dhidi ya mfumo wa siasa za kimaeneo.

Huku hayo yakiendelea, Umoja wa Ulaya unajiandaa kwa namna nyingine kuijibu Urusi iwapo itazidisha hatua zake za kuivuruga Ukraine ingawa bado haujui hasa kile ambacho Urusi inapanga kukifanya.

Afisa mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa amesema mazungumzo ya Marekani na Urusi hayakuwa na matokeo makubwa lakini milango ya majadiliano na rais Vladimir Putin bado iko wazi kupitia kwa viongozi wa Ujerumani na Ufaransa.

Chanzo hicho kimesema Umoja huo pia unatarajia kuamua kuhusiana na msaada zaidi wa uchumi mkubwa na kisiasa nchini Ukraine katika wakati ambapo bado kuna mvutano miongoni mwao kuhusiana na vikwazo dhidi ya Urusi wakati baadhi wakisema hatua hiyo itazidisha mzozo huku wengine wakiunga mkono vikwazo hivyo.

Je, huenda Putin atakubaliana na magharibi kuhusu masharti yake ya kiusalama?

Polen UK Boris Johnson
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson aahidi kuzungumza na rais Joe Biden wa Marekani kusaka suluhu ya diplomasia Picha: Daniel Leal/Getty Images

Katika hatua nyingine, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema Ukraine kama taifa huru lina haki ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na uhuru huo hauwezi kupuuzwa tu huku akiahidi kuzungumza na rais wa Marekani Joe Biden siku chache zijazo kusaidia mchakato wa kidiplomasia.

Tukirejea Urusi, mwanadiplomasia wa juu nchini humo Sergey Lavrov amemshauri rais Vladimir Putin hii leo kuendelea kuzungumza na magharibi kuhusiana na masharti ya kiusalama waliyoyawasilisha kwa mataifa hayo. Mwanzoni mwa mkutano baina yao Lavrov amependekeza Moscow kuendeleza majadiliano hayo na Marekani na washirika wake ingawa tayari waliyakataa masharti muhimu zaidi ya Urusi.

Soma Zaidi: Marais wa Marekani na Urusi kuzungumza kwa simu juu ya mgogoro wa Ukraine

Taarifa za ikulu ya Kremlin zilisema baadae kwamba rais Putin ameidhinisha kimsingi, majibu ya wizara hiyo ya mambo ya kigeni kwa mataifa ya magharibi kuhusiana na dhama ya kiusalama ambayo Moscow inaipigania hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Urusi, RIA na kwamba wanadiplomasia wa Urusi wanamalizia majibu hayo kimaandishi.

Mashirika: RTRE/DPAE