Ujerumani yalipiga marufuku vuguvugu la Hezbollah
30 Aprili 2020Tangazo limetolewa na wizara ya ndani ya Ujerumani na limesifiwa na mataifa ya Israel pamoja na Marekani kama hatua muhimu katika kukabiliana na ugaidi.
Tangazo hilo ambalo limetolewa Alhamisi na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer, limejiri mnamo wakati maafisa wa polisi wamefanya misako ndani ya misikiti na maeneo mengine yanayohusishwa na kundi hilo. Misako hiyo ilifanywa katika miji ya Berlin, Dortmund, Munster na Bremen.
Amri nyingine ambayo shirika la habari la Ujerumani DPA limeona, pia imepiga marufuku matumizi ya alama, ishara au nembo za kundi hilo. Aidha wafuasi wa kundi hilo wamepigwa marufuku kuandaa mikutano na mali zao pia zinaweza kukamatwa.
Baada ya misako iliyofanywa Berlin, msemaji wa polisi Thilo Calbitz amesema "Tunafanya operesheni katika maeneo manne hapa Berlin Neukoelln sambamba na marufuku dhidi ya kundi la Hezbollah. Lengo letu ni kubaini ikiwa kuna uhusiano wowote kati ya maeneo haya pamoja na kundi la Hezbollah, ambalo sasa limepigwa marufuku.”
Akizungumza na gazeti la the Bild la Ujerumani, waziri wa ndani wa Ujerumani Seehofer, ameeleza kuwa uamuzi wa kulipiga marufuku kundi hilo ni kuhusiana na wajibu wa kihistoria wa Ujerumani kwa Israel baada ya masikitiko ya Vita Vikuu vya Pili.
Isarel na Marekani zausifu uamuzi wa Ujerumani
Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Israel Katz ameusifu uamuzi wa Ujerumani akisema ni hatua muhimu katika vita dhidi ya ugaidi, huku akiongeza kuwa ana uhakika serikali zenye misimamo ya wastani Mashariki ya Kati pamoja na maelfu ya waathiriwa wa mashambulizi ya Hezbollah pia wameupongeza uamuzi huo.
Balozi wa Marekani nchini Ujerumani Richard Grenell naye ameupongeza uamuzi huo akisema, unaakisi kujitolea kwa mataifa ya magharibi kukabiliana na kitisho kinachosababishwa na Hezbollah, huku akiongeza kuwa kundi hilo haliwezi kuruhusiwa kuendelea kulitumia bara la Ulaya kama eneo salama la kuunga mkono ugaidi nchini Syria na Mashariki ya Kati.
Grenell na Katz wamezitaka nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya, kuiga mfano huo wa Ujerumani.
Hezbollah lapinga uhalali wa taifa la Israel
Vuguvugu la Hezbollah lilianzishwa nchini Lebanon mnamo mwaka 1982. Wanachama wake hutoka katika jamii ya Washia. Vuguvugu hilo linapinga uhalali wa taifa la Israel na limekuwa likitaka taifa la Israel livunjwe. Vuguvugu hilo limeshutumiwa kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Israel.
Maafisa wa usalama nchini Ujerumani wanaamini kwamba takriban watu 1,050 nchini Ujerumani ni miongoni mwa tawi lenye misimamo mikali ya vuguvugu la Hezbollah.
Vyanzo: DPAE, RTRE, AFPE