Ujerumani yapitisha muswada wa mataifa salama Barani Afrika
13 Mei 2016Kwa ujumla, wabunge 422 wa bunge la Ujerumani, wamepiga kura kuonyesha kukubaliana na muswada huo wa kuziainisha nchi hizo tatu zilizopo Kaskazini mwa Afrika kuwa ni salama. Kulikuwa na kura 143 za kupinga mabadiliko hayo ya sheria, wakati wabunge watatu hawakupiga kura zao.
Hatua hiyo itaifanya serikali ya Ujerumani sasa kuongeza juhudi kwenye utaratibu wa kuwarejesha makwao Waalgeria, Wamorocco na Watunisia waliokuwa wakiomba hifadhi nchini Ujerumani.
Hata hivyo, maamuzi haya yanatakiwa kuridhiwa na baraza la juu la bunge la Ujerumani, Bundesrat, kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake. Chini ya sheria ya Ujerumani, wakimbizi wanaotoka katika nchi ambazo zinatambulika kuwa ni salama, hawana haki ya kuomba hifadhi.
Hata hivyo, muswaada huu unaendelea kupingwa vikali na baadhi ya vyama vya siasa na wanaharakati wanaopigania haki za wahamiaji. Miongoni mwao ni Chama cha Kijani. "Hali ya haki za binadamu katika nchi hizo zinazoitwa kuwa ni salama si shwari", mtaalamu wa masuala ya nje wa chama hicho Jürgen Tritin ameliambia gazeti la Ujerumani la Saarbrücker Zeitung.
Takriban watu 26,000 kutoka nchi hizo waliomba hifadhi mnamo mwaka 2015
Ndani ya bunge hilo, Trittin aliendesha kampeni ya kuwataka wawakilishi wa majimbo ya Ujerumani chini ya chama hicho kupiga kura ya kupinga mabadiliko yaliyomo katika muswada huo, utakapowasilishwa tawi la juu la Bunge, linalokuwa na uwakilishi wa serikali.
Serikali ya mseto ya vyama vya Kijani na CDU, inayoongoza jimbo la Baden-Württemberg lililoko Kusini mwa Ujerumani, imeahidi kupiga kura ya kuiunga mkono kanuni hiyo mpya, iwapo tu hakutakuwepo na vikwazo vya kikatiba.
Mwaka 2014, jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na serikali ya mseto ya chama cha kijamii cha SPD na Chama cha Kijani, pia liliunga mkono mpango wa Ujerumani wa kuongeza nchi ambazo ni salama, ambao uliruhusu Serbia, Macedonia na Bosnia na Herzegovina, kuongezwa katika orodha. Uamuzi huo pia ulikumbana na vipingamizi vikali kutoka chama cha Kijani.
Viongozi wa taasisi mbalimbali kubwa za kijamii nao pia wameeleza wasiwasi wao juu ya dhamana ya wanaoomba hifadhi kwa kusema kwamba utaratibu wake unaweza kudhoofishwa na kanuni hiyo.
Huku akiutetea muswada huo, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, amewaondoa wasiwasi, na kusema Ujerumani itaendelea kushughulika na masuala ya kibinadamu.
Kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakimbizi Barani Ulaya, Ujerumani imekuwa ikipata ukusoaji mkubwa katika miezi ya hivi karibuni wa kupunguza idadi ya watu wanaoomba hifadhi. Mwaka jana, Ujerumani ilishuhudia kuingia kwa kiasi ya wakimbizi Milioni 1.1, wengi wao wakitokea Syria na Afghanistan.
Mwandishi: Lilian Mtono/DW
Mhariri: Mohamed Khelef