Ujerumani yarefusha muda wa karantini hadi Februari 14
20 Januari 2021Kansela Merkel na wakuu hao wa majimbo katika mkutano uliofanyika Jumanne jioni walifikia pia uamuzi mpya ambapo sasa watu watalazimika kuvaa barakoa maalumu (PPF2 ) watakapokuwa wanaingia kwenye vyombo vya usafiri wa umma na katika maduka.
Kansela Angela Merkel amesema dalili kubwa zimejitokeza baada ya kudhihirika mabadiliko kwenye virusi vya COVID -19 ambapo aina mpya ya virusi inaenea kwa kasi na miongoni wanaoathirika ni watoto na vijana tofauti na hapo awali. Amesema dalili hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.
Soma Zaidi:WHO yazilaumu nchi tajiri kwa kujilimbikizia chanjo za COVID-19
Kansela Merkel na wakuu wa majimbo yote 16 hapa nchini Ujerumani wamesema amri ya kuvaa barakoa hizo maalum za kimatibabu, badala ya barakoa za kawaida zinazotengenezwa kwa kutumia vitambaa itakuwepo hadi mwisho wa mwezi huu wa Januari.
Idadi ya watu wanaoambukizwa imepungua katika siku za hivi karibuni na idadi ya wagonjwa wanaolazwa katika wodi za wagonjwa mahututi pia imepungua lakini wataalam wa afya wana wasiwasi juu ya uwezekano wa kuenea kwa kasi zaidi aina mpya ya virusi vya corona.
Kansela wa Angela Merkel amesema nchi zote barani Ulaya lazima ziweke juhudi za kupambana na janga la corona vinginevyo, Ujerumani italazimika kuchukua hatua ya kweka sheria kali katika mipaka yake ili kuzuia maambukizi yanazoweza kuingia kutoka nje za nchi. Merkel na wakuu wa majimbo pia wamezitaka kampuni ziendelee kuweka utaratibu wa kuwaruhusu wafanyikazi wao kufanyia kazi nyumbani hadi Machi 15 pale inapowezekana.
Taasisi ya Ujerumani ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza Robert Koch, imesema kufikia siku ya Jumanne idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona hapa nchini Ujerumani iliongezeka kwa asilimia 2.05 sawa na watu milioni 11,369. Watu 989 walikufa hapo jana kutokana na ugonjwa wa COVID -19 Jumla ya watu waliokufa hapa nchini Ujerumani mpaka sasa ni 47,622.
Vyanzo:/DPA/AP