Heiko Maas akutana na Mike Pompeo
4 Oktoba 2018Maas amesema mkutano huo ulihusisha mazungumzo ya kina kuhusu hali nchini Syria huku pande zote zikiwa makini kuzidisha shinikizo kwa suluhu ya kisiasa, na kutaka kuanza mara moja kuandika upya katiba ya Syria. Ujerumani pia imesema itaunga mkono juhudi za Marekani nchini Syria, kukiwemo kupitia misaada ya kibindamau, na kuhakikisha silaha za kemikali hazitumiki.
Waziri Maas amesema mwenzake wa Marekani, Mike Pompeo anaelewa mjadala wa kisiasa nchini Ujerumani kuhusu uwezekano wa kushiriki shambulio la kijeshi la Marekani iwapo kutatokea shambulio lolote la kemikali, na kwamba bunge huenda lisikubali hatua hiyo. Maas amesema zipo njia nyingi za kusaidia kuhakikisha silaha za kemikali hazitumiki na hazipatikani.
Itakumbukwa mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa mara tisa mjini Geneva, yameshindwa kuzileta pamoja pande zinazozozana nchini Syria kusitisha migogoro ambayo imesababisha kuuawa kwa maelfu ya watu na mamilioni kupoteza makaazi yao.
Aidha, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema nchi yake na Marekani zimekubaliana kuhusu haja ya kukabili shughuli za Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, na mpango wa makombora wa nchi hiyo.
Hata hivyo ameendelea kupinga uamuzi wa Marekani kujiondoa katika mkataba wa nyuklia na Iran wa mwaka 2015, akiongeza kuwa Ujerumani inataka kudumisha makubaliano hayo ya nyuklia na Iran kwa kuwa vitu vingine vyote haviwezi kuleta maendeleo, na hali huenda ikawa mbaya zaidi.
Marekani chini ya utawala wa aliyekuwa Rais Barrack Obama iliingia katika makubaliano hayo na Iran pamoja na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi. Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa walisema Iran iliafikia vigezo vyote vya mkataba huo, ambapo ilisitisha shughuli za kinyuklia ili kupunguziwa vikwazo.
Vikwazo vya Marekani Iran
Marekani imetishia kuziwekea vikwazo kampuni ambazo zinafanya biashara na Iran. Mwezi uliopita Umoja wa Ulaya ulisema unashughulikia taasisi ya kisheria ambayo itaziwezesha kampuni kadhaa kufanya biashara na Iran, na kuepuka vikwazo vya Marekani.
Ujerumani na Marekani zinataka Iran ijiondoe Syria, ambapo inaunga mkono utawala wa Rais Bashar al Assad, pamoja na kushirikiana kutafuta suluhu ya kisiasa ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka saba.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/DW/RTRE/AFPE
Mhariri: Gakuba, Daniel