1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yataka kuitulizanisha Iran

5 Januari 2020

Ujerumani imeanza juhudi kuileta Iran kwenye meza ya mazungumzo ili kuzuwia hatua za kulipiza kisasi kufuatia mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya kiongozi wa juu kwenye jeshi la nchi hiyo, Jenerali Qassim Soleimani.

https://p.dw.com/p/3Viul
Heiko Maas Außenminister
Picha: Imago Images/M. Popow

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, amesema anataka kuitisha mazungumzo kati ya Iran na washirika wakuu wa kimataifa kupoza hali ya wasiwasi iliyopo hivi sasa baada ya mashambulizi hayo ya Marekani ya siku ya Ijumaa (Januari 3) yaliyomuua Jenerali Soleimani aliyekuwa ziarani nchini Iraq.

"Hivi karibuni tutafanya kila tuwezalo kuzuwia kuzorota zaidi kwa hali - kwenye Umoja wa Mataifa, kwenye Umoja wa Ulaya na kwenye mazungumzo na washirika wetu kwenye eneo hilo, yakiwemo mazungumzo na Iran," alisema Maas siku ya Jumapili (Januari 5) kupitia gazeti la Bild am Sonntag.

Iran imeapa kulipiza kisasi kwa mauaji hayo ya kamanda wake wa kikosi maalum cha kijeshi cha Quds, ambacho ni tawi la nje la jeshi la Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Maas alisema hali "imezidi kuwa tete na isiyotabirika."

"Kila mmoja lazima afahamu kwamba uchokozi wowote unaweza kusababisha machafuko yasiyoweza kudhibitika na matokeo yasiyofikirika kwenye eneo zima la Ghuba na Mashariki ya Kati na pia kwa usalama wetu barani Ulaya," alisema waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani.

Kassem Soleimani, der Kommandeur der iranischen Al-Kuds-Brigaden
Mauaji ya Jenerali Qassim Soleimani yanahofiwa yataliingiza eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati kwenye machafuko makubwa.Picha: picture-alliance/dpa/Leaders Official Website

Maas pia alizungumzia malengo matatu ya sasa kwenye kuutatuwa mzozo huo. "Kwanza ni kuiepusha hali ya sasa kugeuka vita. Pili ni kuukinga utulivu na utangamano wa Iraq na, tatu, ni kuhakikisha kwamba magaidi wa ISIS hawapati tena nguvu kutokana na uhasama huu uliozuka."

Kwa mujibu wa Maas, kwa sasa hakuna kitisho cha moja kwa moja kwa watalii wa Ujerumani walioko kwenye eneo la Ghuba, lakini hali inaweza kuwa mbaya wakati wowote.

Trump aapa kuiadhibu vikali Iran

Juhudi za kimataifa zinaanza huku Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye binafsi aliagiza mauaji hayo ya Jenerali Soleimani, akiitishia Iran kwamba nchi yake itavishambulia vituo muhimu 52 kwa Iran endapo Jamhuri hiyo ya Kiislamu itaamuwa kulipiza kisasi.

Akitumia jukwaa lake maarufu la mtandao wa Twitter, Trump ameandika kwamba Marekani itajibu "kwa haraka na kwa nguvu sana", ikiwa Iran itachukuwa hatua za kulipiza kisasi. 

Msururu huo wa twita za vitisho ulitanguliwa na Ikulu ya Marekani kuwasilisha rasmi mbele ya baraza la Congress ilani ya mashambulizi ya ndege isiyo rubani yaliyomuuwa Jenerali Soleimani.

Sheria za Marekani zinataka bunge lifahamishwe ndani ya kipindi cha saa 48 pale jeshi la Marekani linapotumwa kwenye mzozo unaohusisha silaha au hali inayoweza kupelekea vita.

Wachambuzi wengi wanasema kuwa kimsingi tayari Marekani imetangaza vita dhidi ya Iran, na iliyobakia ni juu ya Iran kama itaingia vitani au la.