1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasisitiza uchaguzi 2024 Mali kubakisha wanajeshi

16 Desemba 2022

Vikosi vya Ujerumani vitabakia Mali hadi 2024 pale tu utawala utakapoviruhusu kuendesha shughuli zake kwa uhuru, na uchaguzi kufanyika mwaka 2024, amesema waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht.

https://p.dw.com/p/4L4ki
Mali Besuch Verteidigungsministerin Lambrecht und Sadio Camara
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Lambrecht amesema uwepo wa Ujerumani nchini Mali unategemea kuweza kutimiza makubaliano ya operesheni, kutimiza malengo yao ndani ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, operesheni ya uchunguzi ambayo alisema kwa bahari mbaya haijawezekana kwa wiki kadhaa.

Lambrecht ndiye waziri wa kwanza mwandamizi wa serikali ya Ujerumani kufanya ziara nchini Mali tangu Berlin ilipotangaza mwezi uliopita, mipango ya kukomesha ushiriki wake katika ujumbe wa MINUSMA.

Waziri huyo wa Ujerumani alisema sharti jengine ni kwamba Bamako lazima iheshimu ahadi yake ya kufanya uchaguzi mwezi Februari 2024 ili kupisha utawala wa kiraia.

Verteidigungsministerin Lambrecht in Mali
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht akiwa na mwenzake wa Mali Kanali Sadio Camara katika wizara ya ulinzi ya Mali, Desemba 15, 2022.Picha: Michael Kappeler/dpa

Mali imekuwa ikikabiliana na uasi wa makundi ya itikadi kaliya Kiislamu tangu 2012, ambapo maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu kuyakimbia makaazi yao.

Serikali ya Ujerumani imechukuwa uamuzi wa kuendelea kuunga mkono mchakato wa mpito hadi Mei 2024, lakini Lambrecht, ambaye alikuwa anakutana na mwenzake wa Mali Kanali Sadio Camara, alisema masharti ya msaada huu lazima yatimizwe kikamilifu.

Kwa upande wake, waziri wa ulinzi wa Mali Kanali Sadio Camara alitoa wito wa kuheshimiwa kwa uhuru wa Mali, na kusema amefurahishwa kwamba uondokaji wa wanajeshi wa Ujerumani umepangwa na kutoa nafasi kwa mazungumzo na Bamako.

Alisema anatofautisha hilo na uondoaji wa wanajeshi wa Ufaransa mwezi Agosti,  wakati Ufaransa ilipoondoa wanajeshi wake nchini humo bila uratibu na serikali ya Mali.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilisema ilikuwa imefanya uamuzi huo kutokana na madai ya Mali kutumia mamluki kutoka kundi la kijeshi la Urusi, la Wagner.

Ujerumani Kupeleka wanajeshi wake Niger

Soma pia: Mali yaishtumu Ufaransa kwa ukiukaji wa anga lake kupeleleza wanajeshi

Mali inakanusha madai hayo, na kukiri tu kuhusu msaada wa wakufunzi kutoka Urusi. Lambrecht alisema Ujerumani inao wanajeshi 1,100 nchini Mali.

Ujerumani ni nchi ya saba kuamua katika miezi ya karibuni kusitisha au kusimamisha ushiriki wake katika ujumbe wa MINUSMA nchini Mali, ambayo imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti 2020, na kufuatiwa na mangine Mei 2021.

Chanzo: Mashirika