Ujerumani yawaomba radhi Watanzania kwa madhila ya Ukoloni
1 Novemba 2023Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ameomba radhi kwa Watanzania kwa yale yaliyofanywa dhidi yao wakati wa utawala wa ukoloni wa Kijerumani nchini humo.
Rais Steinmeier ambaye yuko ziarani nchini Tanzania, amezungumzia kusikitishwa kwake na kile alichokiita fedheha ya uhalifu uliofanywa na Ujerumani wakati ilipokuwa ikiitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki,enzi ya Ukoloni.
''Ningependa kuomba msamaha kwa kile Wajerumani walichowafanyia wazee wenu hapa'' Hayo ndiyo maneno aliyoyazungumza rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alipoyatembelea makumbusho ya Maji Maji yaliyoko katika mji wa Kusini mwa Tanzania wa Songea.
Na akazungumzia namna alivyofedheheshwa na uhalifu huo akisema anafahamu jinsi Watanzania ambavyo bado wanabeba mzigo mkubwa kwenye mioyo yao kutokana na madhila hayo huku pia akitambuwa kwamba kilichotokea ni unyama unaoendelea kuviathiri vizazi vingi pamoja na familia.
Tanzania ambayo wakati huo ikifahamika kama Tanganyika ilikuwa kile kilichoitwa Afrika Mashariki ya Ujerumani ikizijumuisha Burundi,Rwanda,Tanganyika na sehemu ya Msumbiji.
Tanganyika ikashuhudia moja ya vita vilivyosababisha umwagaji mkubwa wa damu katika historia ya ukoloni kati ya mwaka 1905 mpaka 1907.
Rais huyo wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeier pamoja na kueleza fedheha iliyosababishwa na madhila hayo amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania kuelekea mchakato wa pamoja wa kuyaangalia madhila ya kihistoria,huku akitilia mkazo kwamba kilichotokea ni historia ya pamoja kati ya Ujerumani na Tanzania inayowahusisha wazee waliotangulia wa pande zote mbili.
Ameahidi kuufikisha ujumbe nchini Ujerumani kwa yaliyotokea ili watu wengi zaidi nchini Ujerumani wayafahamu. Kadhalika aliwaahidi Watanzania kwamba atahakikisha kwamba Wajerumani watakuwa tayari kuyatafuta majibu kwa pamoja na Watanzania ya maswali ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na ambayo yanawakosesha usingizi Watanzania.
Ziara yake katika makumbusho ya vita vya Majimaji imefanyika katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania baada ya hapo jana pia kutangaza kufungua milango ya kurudishwa kwa vitu vya urathi wa kale vilivyoibwa enzi ya Ukoloni. Ujerumani iko tayari kwa ushirikiano kwaajili ya kurudishwa kwa vitu vya kale vya sanaa pamoja na mabaki ya binadamu.