1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawatuliza Waturuki

22 Julai 2017

Jamii ya Waturuki wanaoishi Ujerumani imehakikishiwa kuwa ni sehemu ya nguzo ya taifa licha ya mahusiano magumu yaliyopo kati ya Ujerumani na Uturuki.

https://p.dw.com/p/2h0qd
Berlin Außenminister Sigmar Gabriel zur Lage in der Türkei
Picha: Getty Images/S. Gallup

Baada ya Ujerumani kutangaza mageuzi katika  sera ya misaada na uchumi dhidi ya Uturuki, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel katika barua yake ya wazi amewatolea wito wananchi wenye asili ya Kituruki waliopo Ujerumani kuzingatia uhusiano mwema na urafiki kati ya Wajerumani na Waturuki alioutaja kuwa ni hazina kubwa. 

Hata hivyo waziri Gabriel kwenye barua hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Bild  amesema, Serikali ya Ujerumani haiwezi kunyamaa kimya wakati ambapo raia wake wanakamatwa nchini Uturuki.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amewahakikishia  raia wa Uturuki au raia wa Ujerumani wenye asili ya Kituruki walio ndani ya Ujerumani kwamba hatua zilizochukuliwa haziwalengi wao moja kwa moja.

Baada migogoro kadhaa kati ya serikali ya Ujerumani na Uturuki na hatimaye kukamatwa mwanaharakati wa haki za binadamu wa Ujerumani Peter Steudtner, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imetoa tahadhari kwa raia wake juu ya kufanya safari nchini Uturuki.

Deutschland | Solidaritätsveranstaltung für den in der Türkei inhaftierten Journalisten Deniz Yücel
Mwanahabari Deniz Yucel anazuiliwa UturukiPicha: DW/T. Yildirim

Gokay Sofuoglu, mwenyekiti wa Jamii ya Kituruki nchini Ujerumani, ameyakaribisha maneno ya maridhiano aliyoyatoa Gabriel. Ameliambia gazeti la Wlet am Sonntag kuwa "ni lazima tusiruhusu kutenganishwa hapa Ujerumani. Watu wenye asili ya Kituruki wanapaswa kuiangazia Ujerumani”.

Hatua za kiuchumi

Gabriel amesema msaada wa kiuchumi na hakikisho la uuzaji bidhaa nchini Uturuki vitatathminiwa chini ya mabadiliko hayo. Aidha ameapa kuushinikiza Umoja wa Ulaya kuhusu ahadi yake ya msaada kwa Uturuki, ambayo imekuwa katika mazungumzo ya kujiunga na umoja huo kwa miaka mingi.

Gabriel alimkosoa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa "kuyatelekeza maadili muhimu ya Umoja wa Ulaya kwa kuwazuilia wanaharakati na namna alivyojibu jaribio lililoshindwa la mapinduzi, ambapo zaidi ya watu 50,000 waliwekwa jela wakisubiri kesi zao na 150,000 wakafutwa au kuachishwa kazi kwa muda wakiwemo wanajeshi, maafisa wa polisi, walimu, majaji na watumishi wengine wa umma.

Mshauri wa masuala ya haki za binaadamu Peter Steutdner ndiye raia wa karibuni wa Ujerumani kuzuiliwa na maafisa wa Uturuki. Wanahabari Deniz Yucel na MESALE Tolu pia waliwekwa kizuizini hadi muda usiojulikana kwa tuhuma sawa na hizo za kuwa na mahusiano na makundi ya kigaidi.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Salim-Mtullya, Zainab Aziz