Ujerumani yaweka masharti mapya kudhibiti COVID-19
19 Novemba 2021Hayo yanajiri wakati taifa hilo likipambana na wimbi la nne la maambukizi ambapo ndani ya saa 24 zilizopita, zaidi ya watu 65,000 walirekodiwa kuambukizwa.
Chini ya mpango huo mpya, watu ambao wamechanjwa kikamilifu au waliopona baada ya kuugua covid-19, ndio wataruhusiwa kuingia katika kumbi za starehe, burudani, utamaduni, viwanja vya michezo na migahawa ya vyakula, ikiwa viwango vya maambukizi vitaendelea kuwa juu.
Ikiwa maambukizi yatazidi kuwa juu zaidi, basi hata wale ambao wamechanjwa au waliopona baada ya kuugua watalazimika kuonyesha matokeo ya vipimo kuthibitisha kwamba hawajaambukizwa ndipo waruhusiwe katika maeneo ya huduma za umma.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kwa hakika nchi iko katika hali tete zaidi na wakati umewadia wa kuchukua hatua.
"Leo tumefikia makubaliano, ambayo ni kutokana na ombi la wakuu wa majimbo kwamba wafanyakazi wote katika vitio vya wazee na uuguzi, wapewe chanjo. Hii inamaanisha kwamba serikali ya shirikisho itafanya maamuzi hivi karibuni. Bila shaka hili ni tangazo muhimu,” amesema Merkel.
Wito wa chanjo zaidi kwa wafanyakazi wote hospitalini
Mwenyekiti wa Baraza la wakuu wa majimbo ya Ujerumani Hendrik Wuest amesema wafanyakazi katika sekta mbalimbali ikiwemo hospitalini na vituo vya kuwahudumia wazee pia watatarajiwa kuchanjwa.
Wuest ameahidi juhudi za kitaifa kwa watu kupata chanjo, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtu anapata dozi ya tatu ya ziada ya chanjo, miezi mitano baada ya chanjo zao za awali dhidi ya COVID-19.
Inatarajiwa kwamba katika wiki chache zijazo, chanjo itaidhinishwa kwa hata watoto walio na umri wa kuanzia miaka mitano. Kwa sasa Ujerumani hutoa tu chanjo za COVID-19 kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 12.
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa serikali ya shirikisho na wale wa majimbo yatahitaji kuidhinishwa kuwa sheria. Baadhi katika ngazi ya shirikisho na mengine katika ngazi ya majimbo.
Mkutano huo ulifanyika saa chache baada ya bunge la Ujerumani kupitisha sheria mpya iliyoainisha kanuni za kufuata ili kudhibiti janga la Corona.
Watakaokiuka masharti kupigwa faini kubwa
Ikiwa makubaliano hayo yatapitishwa, basi masharti mapya yatatanuliwa hadi maeneo ya kazi, usafiri wa umma na vituo vya wazee lakini hayajapendekeza shule au biashara kufungwa.
Kulingana na mpango mpya, watakaokiuka masharti watapigwa faini kubwa.
Hapo jana taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Ujerumani Robert Koch, ilitangaza maambukizi mapya ya corona ya jumla ya watu 65,371 ndani ya saa 24 zilizopita. Hiyo ikiwa ongezeko la juu zaidi, kuwahi kurekodiwa Ujerumani.
Mkuu wa taasisi ya Robert Koch Lothar Wieler, ametahadharisha kuwa huenda msimu wa Krismasi usiwe wa kupendeza ikiwa hatua hazitachukuliwa sasa.
(DPAE)
Mhariri: