Ujumbe wa Afrika katika vita vya Ukraine kuanza mwezi huu
6 Juni 2023Viongozi wa Afrika wanaotaka kusimamia juhudi za amani katika vita vya Ukraine wanatarajiwa kuanza ujumbe wao katikati ya mwezi huu. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mwezi uliopita alisema Rais wa Urusi Vladmir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walikubaliana kila mmoja kuipokea timu ya amani ya Kiafrika yenye wajumbe sita. Taarifa kutoka ofisi ya Ramaphosa imesema leo kuwa viongozi wa Afrika waliokutana jana walikubaliana kuwa wataanzisha mazungumzo na Putin na Zelensky kuhusu vipengele vya kusitishwa mapigano na kupatikana amani ya kudumu katika kanda hiyo. Taarifa hiyo hata hiyo haikutoa tarehe kamili ya kufanyika ziara ya wajumbe hao wa Afrika nchini Urusi na Ukraine. Ofisi ya Ramaphosa imesema mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi zinazohusika zitakamilisha vipengele vya mpango wa amani. Ujumbe huo uliotangazwa na Ramaphosa mwezi uliopita, unajumuisha marais wa Jamhuri ya Kongo, Misri, Senegal, Misri, Afrika Kusini, Uganda na Zambia.