Ujumbe wa Marekani wataka rais kukabidhi madaraka kwa amani
19 Agosti 2022Baada ya mkutano wake na Rais Kenyatta, pamoja na wagombea wawili wa kuu wa urais, Raila Odinga na William Ruto Alhamis, Coons aliliambia shirika la habari la AP kwamba alitiwa moyo katika mikutano yote mitatu kwa kusikia misimamo ya wito wa utulivu na kuheshimu michakato ya kisheria iliyoko katika katiba ya mwaka 2010. Coons ameongeza kuwa mazungumzo hayo yalihusu utawala wa kisheria, umuhimu wa uchaguzi huru na haki na kukabidhi madaraka kwa amani.
Marekani inapaswa kujifunza kutoka Kenya
Seneta Coons ameongeza kuwa ni wazi Marekani imekuwa na wakati mgumu sana katika masuala ya uchaguzi katika muda wa miaka michache iliyopita akimaanisha shambulizi la Januari 6 mwaka 2021 dhidi ya jengo la bunge la nchi hiyo wakati aliyekuwa rais Donald Trump alijaribu kubaki madarakani akiongeza kuwa kuna mambo wanapaswa kujifunza kutoka Kenya.
Baada ya mkutano huo na Rais Kenyatta, Coons aliongeza kuwa anampongeza rais huyo kwa kuheshimu katiba na kuondoka madarakani baada ya mihula miwili. Aliongeza kuwa walizungumzia baadhi ya majukumu muhimu ambayo ametekeleza kikanda kusaidia katika mazungumzo nchini DRC, kusaidia katika mazungumzo nchini Ethiopia na kumhimiza Rais Kenyatta kufikiria kuhusu njia baada ya urais wake kukamilika ambapo anaweza kuendelea kuchukua jukumu la kujenga amani ya kikanda.
Coons amesema hakwenda Kenya kutafuta kitu kama makubaliano ya kushiriki katika uongozi wa pamoja ambayo Kenyatta na Odinga walikuwa nayo na kumaliza miezi ya mivutano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ambao matokeo yake yalibatilishwa na mahakama ya juu kutokana na kasoro za uchaguzi, hii ikiwa mara ya kwanza kwa hatua hiyo kuchukuliwa barani Afrika.
Kenyatta asema Kenya itadumisha mfano wa kuigwa wa demokrasia
Taarifa kutoka ofisi ya rais, imesema kuwa Kenyatta amemwambia Coons kwamba Kenya itadumisha nafasi yake ya kuwa mfano wa kuigwa wa demokrasia barani Afrika kwa kudumisha amani wakati wa kipindi hicho cha kukabidhi madaraka.
Kenyatta alikuwa amemuunga mkono Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9 baada ya kukosana na naibu wake William Ruto ambaye alishinda kinyang'anyiro hicho cha urais kwa kura chache. Kiongozi huyo anayeondoka madarakani bado hajampongeza hadharani Ruto, ambaye amehudumu kama naibu rais tangu 2013 na kwa muda mrefu alikuwa akichukuliwa kama mrithi wa Rais Kenyatta.