1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukatili wa wasichana katika nchi za Asia

17 Januari 2023

Nchini Kenya, kundi la wasichana na kina mama waliokuwa wameahidiwa na mawakala wao kwamba wangesafirishwa kuenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia wamekwama mjini Nakuru na wanadai wamelaghaiwa na mawakala wao.

https://p.dw.com/p/4MKMw
Kenia Mombasa
Picha: Halima Gongo/DW

Haya yanajiri huku serikali iliyoingia mamlakani nchini humo ikionyesha juhudi za kukomesha ukatili unaotendewa Wakenya wanaokwenda kutafuta ajira katika mataifa ya Mashariki ya Kati. 

Kina mama na wasichana kutoka eneo la Pwani waliwasili katika kaunti ya Nakuru tarehe tano mwezi huu kwa makusudi ya kupata masomo kabla ya kusafirishwa kwenda nchini Saudi Arabia na mawakala wao kufanya kazi. Mabinti hawa wamekuwa katika taasisi inayofamika kama Impact Home Care Institute iliyoko kaunti ya Nakuru, inayotoa mafunzo kwa wahudumu wa nyumbani wanaoelekea katika mataifa ya kigeni. Hata hivyo, wanalalamika kwamba katika muda waliokuwa hapa, haki zao za kimsingi zimekiukwa. Brenda Gakii mkaazi wa eneo la Lamu anaeleza. Wanalalamika kwamba juhudi zao kupata usaidizi kutoka kwa maafisa wa usalama ziliambulia patupu.

Akizungumza na idhaa hii, kamanda wa polisi katika kaunti ya Nakuru Peter Mwanzo, amethibitisha madai haya, na ameeleza kwamba wameingilia kati kuhakikisha kuwa mawakala waliohusika wanawarejesha kina mama na wasichana hao makwao.

Wasichana na kina mama nchini Kenya wanazidi kusafiri katika mataifa ya Mashariki ya kati kutafuta kipato licha ya tahadhari inayotolewa kufuatia ripoti chungu nzima za dhuluma na udhalalishaji katika nchi hizo. Serikali iliyoingia mamlakani imeonyesha jitihada za kuwashughulikia Wakenya wanaopitia mateso katika mataifa ya Mashariki ya kati. Siku chache zilizopita, katibu wa maswala ya ughaibuni Roseline Njogu aliarifu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba Wakenya 257 waliosafiri nchini Saudi Arabia wapo kwenye kituo cha uokozi, maarufu Sakaan wakisubiri kurejeshwa nchini Kenya. Katibu huyo aliyekuwa amezuru taifa la Saudi Arabia, alionyesha picha za mamia ya wasichana na kina mama wakiwa kweney kituo cha uokozi na kutangaza kuwa maafisa wa ubalozi wa Kenya nchini Saudi Arabia wameagizwa kuanza taratibu za kuwarejesha nyumbani Wakenya waliokwama nchini Saudi Arabia. 

Serikali vilevile imetakiwa kuchukua hatua dhidi ya mawakala wanaowasafirisha Wakenya kutafuta ajira kwenye mataifa hayo na kisha kuwatelekeza mikononi mwa waajiri wa kigeni wanaowadhulumu.

Wakio Mbogho/DW Nakuru