1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukiukaji wa haki za binaadamu Yemen uchunguzwe

27 Januari 2016

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuzingatia kuundwa tume ya kimataifa ili kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binaadamu na pande zote zinazohusika katika mzozo wa Yemen

https://p.dw.com/p/1HkU3
Jemen, Soldaten nach Angriff
Picha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na jopo la watalaamu la Umoja wa Mataifa linalofuatilia vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo ya jopo la watalaamu la Umoja wa Mataifa pia inasema kuwa raia Yemen, ambalo ni taifa maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu, wanateseka kutokana na mbinu za mgogoro huo ambazo “zinajumuisha matumizi ya kunyimwa chakula kama mbinu ya vita”.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia mwaka jana ulizindua mashambulizi ya angani na kisha operesheni ya ardhini dhidi ya waasi wa Houthi wanaomuunga mkono rais wa zamani ambao walikuwa wamekamata maeneo makubwa ya nchi, ukiwemo mji mkuu Sanaa. Waangalizi wameonya kuwa machafuko hayo yanatoa nafasi kwa makundi ya wapiganaji kama vile Dola la Kiislamu kujiimarisha.

Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Zaidi ya watu 5,800 wameuawa na zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu nchini Yemen wanahitaji kwa dharura chakuka, maji na msaada mwingine , kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Juhudi za kufanyika mazungumzo ya amani chini ya upatanisho wa Umoja wa Mataifa yamegonga mwamba kufikia sasa.

Umoja wa Mataifa umeuzungumzia kwa kiasi kikubwa mzozo huo na athari zake katika siku za karibuni. Mapema mwezi huu, serikali ya Yemen ilimfukuza kwa muda mfupi mwakilishi wa haki za binaadamu nchini humo baada ya ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa kusema ilipokea madai kuwa majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia walitumia mabomu ya sumu katika mashambulizi yake.

Katika wakati huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu “kuongezeka” kwa mashambulizi ya angani ya muungano huo unaoungwa mkono na Marekani na akaonya kuwa ripoti za matumizi ya mabomu ya sumu katika maeneo yenye watu wengi kunaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Ripoti hiyo mpya inasema kuwa katika baadhi ya matukio, iligundua kuwa muungano huo uliwalenga raia katika mashambulizi hayo kwa mpangilio. Jopo hilo linasema liliratibu mashambulizi 119, yanayohusiana na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kiutu, huku mashambulizi mengi yakiwalenga raia.

Aidha kuna matukio matatu yanayodaiwa kuwa ya raia waliokuwa wakitoroka mabomu yaliyokuwa yakiangushwa katika makaazi yao na kisha wakafutwa na kupigwa risasi na helikopta. Jopo hilo halikuruhusiwa kwenda Yemen, kwa hivyo lilitegemea picha za satelaiti na vyanzo vingine katika uchunguzi wake.

Ripoti hiyo pia inasema muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umetekeleza jukumu la moja kwa moja katika ueneaji wa silaha nchini Yemen kwa kuyapa silaha makundi yanayoshiriki katika vita bila kuchukua hatua za kuhakikisha uwajibikaji na kuhifadhiwa silaha hizo katika njia iliyo bora.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo