1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukodishaji wa bandari ya Dar es Salaam waibua mjadala

7 Juni 2023

Kumekuwa na mjadala unaoendelea nchini Tanzania kufuatia hatua ya Serikali kuingia makubaliano na ukodishaji wa bandari ya Dar es Salaam na kampuni moja ya kimataifa ifahamikayo DP World ya Dubai.

https://p.dw.com/p/4SISI
Tansania | Hafen in Dar es Salaam
Picha: Xinhua/picture alliance

Mjadala huo unahoji mazingira ya mkataba huo pamoja na vipengele vilivyomo huku baadhi wakionya kuhusu hali hiyo. 

Mjadala huo umeyavutia makundi ya aina mbalimbali kuanzia ndani ya watendaji wa serikali pamoja na wale wapembeni wanaoonyesha ukosoaji wa waziwazi.

Soma pia:Tanzania yasaini mkataba wa reli wa dola bilioni 2.2 na China 

Duru za habari zinaonyesha kuwa serikali ya Tanzania kupitia mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini TPA, imeanzisha majadiliano na kampuni ya usafirishaji mizigo ya Dubai Port ( DP World) inayomilikiwa na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya kuendesha bandari zote zilizoko nchini.

Licha ya mamlaka ya bandari nchini kufafanua kuwa hakuna mkataba wowote uliosainiwa baina ya pande hizo mbili, hata hivyo wale wanaohoji wanasema kitendo cha serikali kuwahisha kupeleka bungeni azimio la kuanzisha majadiliano hayo linazidisha wasiwasi kuhusu yale yanayoweza kufikiwa kwenye mkataba huo.

Upi ukweli kuhusu ukodishaji wa bandari ya Dar es Salaam kwa DP kwa miaka 100?

Tansania | Hafen in Dar es Salaam
Bandari ya Dar es Salaam ikifanyiwa uboreshaji wa gati 1 hadi 7 jijini Dar es Salaam na kampuni ya uhandisi ya China.Picha: Xinhua/picture alliance

Maoni mchanganyiko yameendelea kuugubika mchakato huo ambao pia ulizua majdala bungeni hivi karibuni wakati wizara ya ujenzi na uchukuzi ilipowasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023-2024.

Sehemu kubwa ya wabunge walikosoa mchakato huo wakionyesha wasiwasi na kudai kwamba unaweza kulitumbulkiza taifa katika mazingira yenye utata.

Hata hivyo, waziri wa wizara hiyo, Profesa Makame Mbarawa alitumia muda mwingi kuwaondoa hofu wabunge huku akitaja ufanisi wa baadhi ya bandari duniani zilizoingia ubia na sekta binafsi.

Soma pia: Uganda na Tanzania zasaini mkataba ujenzi wa bomba la mafuta

Kufuatia mkanganyiko huo unaoendelea kujadiliwa nchini, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Freeman Mbowe anakusudia kutoa tamko la awali la chama chake baadaye leo jioni.

Ama, ofisi ya msemaji wa serikali  inakusudia kuendesha majadiliano ya wazi kupitia mtandao wa club house kwa ajili ya kulijadili suala hilo hilo, mjadala ambao umepangwa kufanyika leo usiku.