Ukosefu wa ajira kuzidi kuuma kanda ya Euro
25 Julai 2013Utafiti huo wa Shirika la habari la Reuters kwa chumi zilizo katika hatari zaidi katika kanda inayotumia sarafu ya euro, ambao uliwahusisha wataalamu wa uchumi zaidi ya 40, ulifuatia mkutano wa mawaziri wa fedha wa kundi la mataifa 20 yaliyoendelea kiviwanda, pamoja na maafisa wa benki kuu za mataifa hayo siku ya Jumamosi, ambao waliahidi kutoa kipaumbele kwa ukuaji wa uchumi badala ya kukaza mkwiji, ili kufufua uchumi wa dunia.
Uchumi wa mataifa ya kusini mwa kanda inayotumia sarafu ya euro ndiyo umeathirika zaidi na hatua za kubana matumizi, ambazo zimesababisha gharama kubwa za kiuchumi na kibinaadamu kuliko watetezi wake walivyowazia mwaka 2010. Wachumi wanatarajia kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Uhispania na Ugiriki kuendelea kuwa juu ya asilimia 27, na hali hii inaweza kuendelea hivyo hadi mwaka 2015 kwa mujibu wa uchunguzi huo.
Watu milioni 19.3 hawana ajira
Kiwango cha ukosefu wa ajira katika kanda ya euro kilifikia asilimia 12.2 mwezi Mei, na kuwaacha watu zaidi ya milioni 19.3 wakiwa hawana kazi - idadi ambayo ni sawa na jumla ya wakaazi wa nchi za Austria na Ubelgji. Alan MqQauid, mchumi kutoka kampuni ya udalali ya Merrion ya mjini Dublin, anasema hatua za kubana matumizi zisizo na mwisho hazijasaidia, na tatizo la ajira, hasa kwa vijana, linaendelea kuwa kubwa kwa kanda ya euro.
Uchunguzi tofauti wa Shirika la Reuters wiki iliyopita ulilitaja tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kama kitisho kikubwa zaidi kwa uchumi wa kanda ya euro, pamoja na mfumo wake dhaifu wa benki. Angalau utafiti wa hivi karibuni imeonyesha kuwa Ureno na Uhispania zinapaswa kurejea katika njia ya ukuaji wa uchumi mwakani, wakati Ugiriki inaweza kuondokana na uzorotaji uchumi wa miaka sita mwaka 2014, hata kama ukuaji wa moja kwa moja bado ni safari ndefu.
Ireland yaonyesha matumaini
Kwa ujumla mtazamo wa kiuchumi haukuwa na mabadiliko makubwa kutoka utafiti wa mwezi April. Ireland, ambayo mara nyingi huwekwa katika kundi moja na mataifa ya kusini mwa Ulaya kutokana na kuanguka kwa mfumo wake wa benki na nakisi kubwa ya bajeti, imefanikiwa kupata ukuaji wa wastani katika miaka miwili iliyopita, ingawa iliangukia tena katika mdororo mwanzoni mwa mwaka huu.
Wachumi wanatarajia uchumi wake kuongeza kasi mwaka 2014, kwa kuwa na ukuaji wa asilimia 1.9, na kupungua taratibu kwa ukosefu wa ajira. Kwa sasa mauzo ya nje ndiyo tegemeo pakee la uchumi wa uhispania, ambao ulianguka kutokana na kupungua kwa uwezo wa raia kufanya manunuzi na kuchechemea kwa masoko ya nyumba, jambo linalofanya ufufukaji wa uchumi huo kutegemea zaidi namna uchumi wa dunia unavyofanya katika miezi ijayo. Lakini kwa sasa ni Marekani inayoongoza gurudumu la uchumi wa dunia.
Dalili chanya Ugiriki, Ureno nako...
Ugiriki, ambayo ndiyo kitovu cha mgogoro wa madeni wa kanda ya euro, inaelekea kubakia katika mdororo kwa mwaka wa sita mfululizo, uchumi wake ukishuka kwa asilimia 4.5 mwaka huu. Lakini mchumi kutoka taasisi ya utafiti ya IOBE nchini humo, Angelos Tsakanikas alisema picha ya jumla ni ya mchanganyiko, akifafanua kuwa kurejeshwa kwa urari kati ya nakisi ya akaunti ya mapato ya nchi na nakisi ya bajeti, ambazo ziliakisi ugonjwa wa uchumi wa Ugiriki kwa miaka kadhaa kumeonyesha dalili chanya.
Hata hivyo, nchi hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa ya kisiasa. Serikali yake ina wingi mdogo, wakati machafuko ya kiraia yanazidi kuikabili, hasa baada ya mswada wa wiki iliyopita wa kupunguza wafanyakazi 25,000 wa umma katika kipindi cha miezi minane.
Ureno pia imekuwa katika mgogoro wa kisiasa unaotishia kukwamisha juhudi za mageuzi na kuondoka kutoka mpango wa uokozi wa euro bilioni 78 kufikia katikati ya mwaka 2014 kama ilivyopangwa. Hofu ya wawekezaji ilitulizwa mwishoni mwa wiki baada ya rais kusema kuwa hatoitisha uchaguzi wa haraka, lakini matatizo bado yapo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman