Ukosefu wa Mazoezi wachangia matatizo ya kiafya
5 Septemba 2018
Jumla ya watu bilioni 1.4 hawaafikii lengo la idara ya afya ya Umoja wa Mataifa, wa kufanya mazoezi ya angalau dakika 150 au dakika sabini na tano ya kazi ngumu kila wiki. Mtafiti wa WHO Regina Guthold ambayo ndiye mwandishi mkuu wa utafiti huo ulioachapishwa leo, anasema mbali na matatizo makubwa ya kiafya duniani, viwango vya ukosefu wa mazoezi ya viungo havipungui kwa kiasi.
Mataifa ya Uganda na Msumbiji ni miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yana idadi ndogo ya watu wasiofanya mazoezi ambayo ni asilimia 6. Hali hiyo imetokana na sababu kwamba wengi wanajishughulisha na kilimo ambacho huwalazimu kutumia nguvu nyingi.
Kulingana na data hiyo, asilimia 27.5 ya watu wazima hawakufanya mazoezi katika mwaka 2016, ambayo ni upungufu wa asilimia moja tangu mwaka 2001. Mataifa tajiri ya Magharibi na yale ya Amerika ya Kusini kama vile Ujerumani, New Zealand, Marekani, Argentina na Brazil yalirekodi ongezeko katika ukosefu wa mazoezi katika muda huo.
Mataifa ambayo watu hawafanyi mazoezi ni pamoja na yale ya Uarabuni: Kuwait, Saudi Arabia na Iraq. Katika mataifa hayo matatu, ambayo yameorodheshwa ya chini na WHO, watu wanaopungua idadi nusu ya watu wazima wanafanya kiwango kidogo cha mazoezi yanayopendekewa.
WHO inasema, katika mataifa yenye utajiri, watu wanazidi kutokuwa na afya nzuri kwa sababu wanatumia kazi zao na muda wao wa mapumziko wakikaa badala ya kutembea, na kwa kutumia magari sana. Regina anasema, ´´Watu wanaopata kiwango kidogo cha mshahara, katika mataifa yenye mapato madogo, ni asilimia 16 ambao hawafanyi mazoezi. Katika mataifa yenye pato la wastani ni asilimia 28 na mataifa yenye pato kubwa ni asilimia 37. Kwa hivyo muundo huo ni wazi kwamba mataifa yenye utajiri yana watu wengi wasiofanya mazoezi.´´
WHO aidha imelitaja pia taifa la Uchina kuwa mfano bora, ambapo idadi ya raia wanaofanya mazoezi ya nje imeongezeka tangu mwaka 2001.
Mataifa yatakiwa kuboresha miundo msingi
Idara hiyo ya afya imesema kwamba tatizo hilo haliwezi kusuluhishwa tu kwa kuwaeleza watu kufanya mazoezi. Inasema kwamba serikali lazima ihakikishe miundo msingi ipo na inachangia kuongezeka kwa watu wanaotembea kwa miguu na wanaotumia baisikeli kama chombo cha usafiri, pamoja na wanaoshiriki michezo na burudani.
Shirika la WHO limesema wakati mataifa mengi yakiwa na mipango ya kukabili tatizo la watu kutokuwa na shughuli za kufanya mazoezi, ni machache ambayo yametekeleza mipango hiyo katika njia yenye manufaa. Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye jarida la afya la The Lancet, imetokana na utafiti uliofanywa miongoni mwa mwa watu milioni 1.9 katika mataifa 168.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman