Ukosefu wa nyama kwa wakimbizi waongeza biashara ya nyama pori
21 Januari 2008Ukosefu wa nyama katika orodha ya vyakula vya wakimbizi katika nchi za Afrika Mashariki unasababisha kunawiri kwa biashara haramu ya nyama ya wanyama pori hivyo kutishia idadi ya wanyama wa pori na kusababisha tatizo la usalama wa chakula katika jamii za maeneo ya mashambani. Hayo ni kwa mujibu ya ripoti ya mtandao unaochunguza biashara haramu ya wanyama pori ujulikanao kwa jina Traffic.
Ripoti ya mtandao wa Traffic iliyopewa jina la ´Night Time Spinach,´ yaani mchicha wa usiku, kuhifadhi nyama ya wanyama pori na athari za matumizi yake katika kambi za wakimbizi kaskazini magharibi wa Tanzania, inatumia chunguzi zilizofanywa Kagera na Kigoma nchini Tanzania. Eneo hili ni mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa ya wakimbizi duniani na linaloongoza kwa idadi ya wakimbizi barani Afrika.
Nyama ya wanyama pori inauzwa kinyume cha sheria na hupikwa wakati giza linapoingia na huitwa mchicha wa usiku katika kambi nyingi za wakimbizi. Kiwango cha nyama ya pori inayotumiwa katika makambi ya wakimbizi kimesaidia kudhihirisha kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kukidhi mahitaji msingi ya wakimbizi, amesema Dakta George Jambiya, mtayarishi mkuu wa ripoti hiyo. Aidha bwana Jambiya amesema mashirika ya misaada yanaifumbia macho sababu halisi ya uwindaji wa wanyama pori na biashara haramu akiitaja kuwa ukosefu wa nyama katika lishe ya wakimbizi.
Idadi kuwa ya wakimbizi mara kwa mara husababisha uharibifu wa mazingira na kupotea kwa kasi kubwa wanyama pori katika maeneo yaliyoathirika, huku wanyama kama vile sokwe wakikabiliwa na hatari kuwa kutokana na nyama yao kutakikana sana na wateja. Idadi ya vifaru, paa na wanyama wengine wanaokula nyasi imepungua kwa kasi kubwa.
Tangu Tanzania ilipojipatia uhuru mnamo mwaka wa 1961, ziara ya kambi kubwa 20 za wakimbizi zimejengwa karibu na mbuga za wanyama, mbuga za kitaifa au maeneo mengine yanayolindwa. Kufikia mwaka wa 2005 kulikuwa na kambi 13 katika maeneo hayo. Katikati ya miaka ya 1990, kadri tani 7.5 ya nyama haramu ya pori zililiwa kila wiki katika kambi mbili kubwa za wakimbizi.
Shirika la Traffic linasema katika ripoti yake kwamba wakimbizi wanaadhibiwa mara mbili. Haki yao ya kupata huduma za kibinadamu mara kwa mara wananyimwa na juhudi zao za kibinafsi kuzifikia huduma hizo zinachukuliwa kama uhalifu. Kinyume cha mambo lakini ni kwamba misaada ya kiutu kwa watu waliolazimika kuyahama kazi yao nchini Croatia, Slovenia na Serbia katika miaka ya mwanzo ya 90 ilijumulisha nyama ya mikebe.
´Lazima kuna kitu kinachoenda kombo ikiwa wakimbizi waliolazimika kuzikimbia bunduki nchini mwao, wanalazimika tena kuwakimbia wawindaji haramu wa wanyama pori wakati wanapojitafutia chakula,´ amesema Simon Milledge wa shirika la Traffic na mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo kuhusu tatizo la uwindaji haramu linalosababishwa na ukosefu wa nyama katika makambi ya wakimbizi.
Biashara ya nyama pori haina gharama kubwa ikilinganishwa na nyama ya ng´ombe na kwa wakimbizi wengi inakubalika kwa urahisi kitamaduni na huwasaidia kupata kipato. Hiyo ni licha ya sera rasmi ya wakimbizi nchini Tanzania ya kudumaza juhudi za wakimbizi kuweza kujisimamia kimaisha makambini.
Mashirika ya kuwalinda wanyama pori yanaamini ufunguo wa tatizo hili ni kuhakikisha wakimbizi wanapelekewa nyama kutoka vyanzo vinavyokubalika rasmi na vinavyoweza kutosheleza mahitaji yao, pamoja na kuziongezea nguvu sheria katika maeneo hayo.
Dakta Susan Lieberman, mkurugenzi wa mpango wa shirika la kimataifa la kulinda aina mbalimbali za mimea na wanyama, WWF, amesema ukweli unaohuzunisha ni kwamba wale wanaotegemea sana chakula kutoka misituni ndio wanaoathirika sana na kupotea kwa aina mbalimbali ya wanyama na mimea. Aidha mkurugenzi huyo amesema shirika la WWF linayatolea mwito mashirika ya kutoa misaada yahakikishe usalama wa chakula kwa wakimbizi, ikiwa ni pamoja na protini ili kuwapa mwelekeo imara katika siku za usoni.
Kiongozi wa chama cha kulinda viumbe duniani, Dakta Jane Smart, amesema orodha ya viumbe vilivyo hatari barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni kubwa huku asilimia 20 ikisababishwa na baishara haramu ya nyama ya pori.
Kupotea kwa wanyama pori huenda kukasababisha kupotea kwa mapato huku maeneo yakiachwa bila viumbe na hivyo kutowavutia tena wageni. Jambo hili huenda pia lisababishe athari za kiuchumi pamoja na hasira miongoni mwa wakaazi wa maeneo hayo.
Ripoti hiyo inapendekeza ushirikiano wa karibu kati ya mashirika ya wanyama pori na ya kutoa misaada ya kiutu, ambayo tayari yamepata ufanisi katika kukabiliana na athari za kimazingira kwa kambi za wakimbizi kama vile ukataji miti ovyo.