Ukraine na Urusi zashambuliana kwa droni usiku kucha
12 Oktoba 2024Mamlaka za Urusi zimesema mapema leo kuwa zimezidungua droni 47 zilizorushwa kutoka Ukraine. Kwa upande wake Ukraine nayo imearifu kwamba imefanikiwa kuziangamiza droni 24 zilizorushwa na Urusi zilizolenga kuishambulia nchi hiyo.
Jeshi la wanaanga la Ukraine limesema pia kuwa Urusi ilirusha makombora mengi kutokea katika eneo la mpaka la Belgorod, ingawa hakukuwa na taarifa juu ya aina ya makombora yaliyotumika kwenye mashambulizi hayo.
Soma zaidi. Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana
Mamlaka za Ukraine zimesema mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu katika miji ya Sumy, Poltava, Dnipropetrovsk, Mikolayev na Kherson.
Ukraine pia ilisema imeshambulia ghala la mafuta katika eneo la Lugansk linalokaliwa na Urusi na kulichoma moto ingawa Urusi haijathibitisha juu ya shambulio hilo.
Vikosi vya Urusi vimepiga hatua katika uwanja wa mapambano upande wa mashariki mwa Ukraine na vimeilenga gridi ya umeme ya Ukraine wakati nchi hiyo ikikabiliwa na msimu mgumu zaidi wa baridi tangu Urusi ilipoivamia Februari 2022.