1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yaashiria utayari wa kuzungumza na Urusi kuhusu vita

Josephat Charo
24 Julai 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amemwambia waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi katika mazungumzo yaliyofanyika mji wa kusini wa Guangzhopu kwamba Ukraine iko wazi kwa mazungumzo na Urusi.

https://p.dw.com/p/4igj8
China Guangzhou | Dmytro Kuleba na Wang Yi
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi Picha: Lu Hanxin/AP/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje na mwanadiplomasia mkuu wa Ukraine Dmytro Kuleba amemwambia waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi katika mazungumzo yaliyofanyika mji wa kusini wa Guangzhopu kwamba Ukraine iko wazi kwa mazungumzo na Urusi ikiwa serikali ya mjini Moscow iko tayari kufanya mashauriano kwa nia njema.

Kuleba amesema hilo ni jambo ambalo haoni ushahidi wowote kwa wakati huu kwa upande wa Urusi. Waziri Kuleba ndiye afisa wa cheo cha juu kabisa wa Ukraine kuzuru China tangu uvamizi wa Urusi Februari 2022 na kufanya mazungumzo na waziri Wang Yi kwa zaidi ya kipindi cha masaa matatu.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema Kuleba amesisitiza kuwa serikali ya mjini Kyiv iko tayari kukaa katika meza ya mazungumzo na Urusi wakati itakapokuwa tayari kufanya mashauriano, lakini akasisitiza pia kwamba hakuna utayari huo kwa upande wa Urusi kwa sasa.