Ukraine yafanya mashambulizi ya droni katika eneo la Crimea
17 Mei 2024Shambulizi kubwa la droni za Ukraine katika eneo la Crimea mapema leo, limesababisha kukatika kwa nguvu za umeme katika mji wa Sevastopol na kuteketeza kiwanda cha kusafishia mafuta kusini mwa Urusi. Haya yamesemwa leo na mamlaka ya Urusi.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa mfumo wa ulinzi wa anga umedungua droni 51 katika eneo la Crimea, na nyingine 44 katika eneo la Krasnodar huku sita zikidunguliwa katika eneo la Belgorod.
Soma: Urusi na Ukraine zashutumiana mashambulizi ya droni
Wizara hiyo imeongeza kwamba ndege za kivita za Urusi pamoja na boti za doria pia zimeharibu droni sita katika bahari nyeusi.
Gavana wa Sevastopol Mikhail Razvozhayev, amesema shambulizi hilo limeharibu kiwanda cha umeme na kuongeza kuwa itachukuwa siku nzima kurejesha kikamilifu huduma hiyo.
Razvozhayev pia ametangaza kuwa shule mjini humo zitafungwa kwa muda.