Ukraine yaifungulia kesi ya 9 Urusi kwenye Mahakama ya Ulaya
23 Februari 2021Umoja wa Ulaya umeamuwa kuanzisha vikwazo vipya dhidi ya maafisa wa Urusi wanaohusika na kufungwa jela kwa mpinzani wa Rais Vladimir Putin, Alexei Navalny, ambaye sasa anatumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Mkuu wa sera za nje za Umoja huo, Josep Borrell, amesema uamuzi huo uliofikiwa usiku wa jana (Februari 22) unatokana na mawaziri wa mambo ya kigeni kujiridhisha kuwa Urusi imeamuwa kuchukuwa njia ya kujitenga na Ulaya na ya kidikteta katika utawala wake.
"Kuna makubaliano ya pamoja kwenye Baraza la Umoja wa Ulaya kwamba Urusi inaelemea zaidi kwenye kuwa dola la kikandamizaji na kujiondowa kabisa kwenye misingi ya Ulaya. Mawaziri kwa kauli moja wamevitafsiri vitendo vya hivi karibuni vya Urusi kama ni ishara ya wazi ya kutokutaka kushirikiana na Umoja wa Ulaya." Alisema Borrell mbele ya waandishi wa habari mjini Brussels.
Ukraine yafunguwa kesi ya tisa dhidi ya Urusi
Hayo yakijiri, Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya imekiri kupofungua kesi iliyowasilishwa na Ukraine dhidi ya Urusi, ambayo inaitaja Urusi kwamba mdhamini wa mauaji dhidi ya wakosoaji wake, ama iwe ndani au nje ya ardhi yake, hata katika mazingira ambapo hakuna vita vya silaha baina ya mataifa hayo na Urusi.
Gazeti la Europeiska Pravda la Ukraine limeandika kwamba malalamiko kwenye kesi hiyo yanajumuisha kesi inayomuhusu mkosoaji mkubwa wa Ikulu ya Kremlin, Alexei Navalny, ambaye alishambuliwa kwa sumu aina ya Novichok mwaka jana, huku serikali ya Urusi ikitajwa kuhusika.
Hii ni kesi ya tisa kufunguliwa na Ukraine dhidi ya Urusi kwenye Mahakama hiyo ya Haki za Binaadamu ya Ulaya, ambayo husikiliza malalamiko juu ya uvunjaji wa mkataba wa haki za binaadamu wa Ulaya.
Naibu Waziri wa Sheria na Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Ukraine, Ivan Lischyna, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kesi zote walizofunguwa zina ushahidi mzito dhidi ya Urusi, ikiwemo ya Urusi kushindwa kuchunguza na badala yake kuwaficha watu ambao walilazimika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kesi nyengine zinahusiana na kuangushwa kwa ndege ya Malaysia chaa MH17 kwenye anga la mashariki mwa Ukraine mnamo Julai 2014, uvunjaji wa haki wa binaadamu kwenye mkoa wa Crimea, ambao Urusi iliutwaa kutoka Ukraine mwaka 2014 na pia kushikiliwa kwa meli tatu za jeshi la wanamaji la Ukraine katika Mlango Bahari wa Kerch mwaka 2018.