1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yataka Urusi iwekewe vikwazo vipya

Zainab Aziz Mhariri: Sylvia Mwehozi
3 Aprili 2022

Ukraine siku ya Jumapili imewalaumu wanajeshi wa Urusi kwa kutenda uhalifu wa kivita baada ya kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki katika mji wa Bucha ulio karibu na mji mkuu wa Kyiv.

https://p.dw.com/p/49OzD
Ukraine - Explosion in Erdölraffinerie in Odessa
Picha: Manuel Bruque/Agencia EFE/imago images

Waandishi wa habari wa shirika la AFP wamesema waliiona takriban miili 20, ya watu waliokuwa wamevaa kiraia, ikiwa imetapakaa katika barabara moja kwenye mji huo wa Bucha. wamesmema mwili mmoja ulikuwa ni wa mtu aliyefungwa mikono yake nyuma ya mgongo wake kwa kitambaa cheupe, na kulikuwa na pasipoti yake ya Ukraine iliyoachwa wazi kando ya mwili wake.

Wahanga wa mashambulizi katika mji mwa Bucha nchini Ukraine
Wahanga wa mashambulizi katika mji mwa Bucha nchini UkrainePicha: Mykhaylo Palinchak/ZUMA Press/dpa/picture alliance

Meya wa mji wa Bucha Anatoly Fedoruk amesema watu wote hao waliuawa kwa kupigwa risasi, akiongeza kuwa miili mingine 280 ilikuwa imezikwa kwenye makaburi ya pamoja katika eneo jingine kwenye mji huo Bucha.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameyaita kuwa ni mauaji yaliyokusudiwa na amezitaka nchi za G7 kuiwekea Urusi vikwazo vikali zaidi mara moja.

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel Picha: Kenzo Triboulliard/AFP

Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya unaisaidia Ukraine na mashirika yasiyo ya kiserikali kukusanya Ushahidi kwa ajili ya kupeleka malalamiko katika mahakama za kimataifa.

Naye makamu wa kansela na waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amesema uhalifu wa kivita umetekelezwa mjini Bucha na ametoa wito wa kuwekwa vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi.

Soma zaidi:Ukraine yachukua udhibiti wa eneo la Kyiv kutoka kwa Warusi

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague tayari imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo uhalifu wa kivita umefanyika nchini Ukraine.

Kwa upande wake shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema limeorodhesha matukio ya wanajeshi wa Urusi wanaofanya uhalifu wa kivita dhidi ya raia katika maeneo wanayoyakalia kimabavu ya Chernigiv, Kharkiv na Kyiv, ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji.

Mapema Jumapili milipuko iliripotiwa kutokea katika mji muhimu wa pwani wa Odessa nchini Ukraine. Mji huo ulishambuliawa kwa roketi mbili ambapo Urusi imedai kuwa imefanya mashambulizi hayo yaliyolenga baadhi ya miundombinu katika mji huo.

Moshi mzito baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta kushambuliwa katika mji wa Odessa.
Moshi mzito baada ya kiwanda cha kusafisha mafuta kushambuliwa katika mji wa Odessa.Picha: Manuel Bruque/Agencia EFE/imago images

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema majeshi yake yamekilenga kiwanda cha kusafisha mafuta na sehemu nyingine tatu za kuhifadhi mafuta katika eneo hilo la Odessa ambalo kwa mujibu wa Urusi Ukraine ilikuwa ikilitumia kwa shughuli za ugavi kwa wanajeshi wake.

Mashambulizi hayo yametokea huku mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths akitarajiwa mjini Moscow kisha ataelekea Kyiv kutafuta kusitishwa kwa mapigano, ambayo kwa makadirio ya Ukraine yamesababisha vifo vya watu wapatao 20,000.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths.Picha: UN/Mark Garten

Takriban raia milioni 4.2 wa Ukraine wameikimbia nchi yao tangu Urusi ilipoivamia mnamo Februari 24, huku takriban watu 40,000 wakimiminika katika nchi jirani katika muda wa saa 24 zilizopita kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR.

Vyanzo:AFP/AP