1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yasema idadi ya raia waliouawa imepindukia 12,000

Sylvia Mwehozi
13 Juni 2022

Zaidi ya raia elfu 12,000 wameuawa hadi kufikia sasa katika uvamizi wa Urusi kulingana na mkuu wa polisi wa Ukraine. Kyiv imezidi kuomba usaidizi wa silaha zaidi ili hiyo iweze kuutetea mji wa Sievierodonetsk.

https://p.dw.com/p/4Cde1
Ukraine Krieg | Lage in der Stadt Severodonetsk | Region Luhansk
Picha: Serhii Nuzhnenko/REUTERS

Katika mahojiano na shirika la habari la Interfax, mkuu wa polisi wa Ukraine Ihor Klymenko amesema kuwa asilimia 75 ya waliouawa ni wanaume, asilimia mbili watoto na waliobakia ni wanawake. "Hawa ni raia, ni watu wasiohusika na jeshi au vikosi vya usalama". Zaidi ya miili 1,500 ilikutwa katika mitaa ya mji mkuu wa Kyiv, baada ya vikosi vya Urusi kujiondoa mwishoni mwa mwezi Machi. Umoja wa Mataifa hadi sasa umerekodi vifo vya watu 4,300.

Vikosi vya Urusi wakati huo, vimeendelea na mashambulizi katika mji wa Sievierodonetskambako mamia ya raia wamechukua hifadhi. Ukraine imezidisha wito wa msaada wa dharura kwa nchi za magharibi kutoa silaha ili iweze kuutetea mji huo ambao, Kyiv inasema unaweza kutoa hatma ya matokeo ya udhibiti wa mji wa mashariki wa Donbas na mustakabali wa vita.

Ukraine | Krieg | Evakuierungen in Lyssytschansk
Wananchi waliohamishwa kutoka LyssytschanskPicha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Waasi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi wamedai kwamba daraja la mwisho linalounganisha mji huo limeharibiwa na hivyo kuwazuia wapiganaji wa Ukraine ndani. Mizinga ya Urusi ilivurumushwa pia katika kiwanda cha kemikali cha Azot, ambako mamia ya raia wamejificha. Kabla ya mji wa Mariupol kudhibitiwa na Urusi mwezi uliopita, mamia ya raia na wanajeshi wa Ukraine walikuwa wamekwama kwa wiki kadhaa katika kiwanda cha chuma cha Azovstal. Maafisa wa Ukraine wanasema kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao unaenea miongoni mwa wakaazi waliosalia.

Zelenskiy asema vikosi vyake vyazidi kushangazaKatika hatua nyingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa wito kwa washiriki wa Jukwaa la kimataifa la kamati ya Wayahudi ya Marekani kuzidisha juhudi zao za kusitisha vita nchini Ukraine. Akizungumza kwa njia ya video kwa washiriki wa kongamano hilo, Zelenskyy alibainisha kuwa Urusi bado ina uwezo wa kutosha kuendeleza vita dhidi ya Ukraine.

"Wakati huo huo, Urusi inatumai kwamba haitawajibika haswa kwa uovu huu wote na kwa mashambulizi yote ya kinyama kwenye majengo ya makazi, hospitali, na makanisa. Urusi bado ina uwezo wa kutosha kutumaini kwamba vita dhidi ya Ukraine na dhidi ya watu vitaendelea, na kupuuza miito ya ulimwengu."

Na wakati huo serikali ya Ukraine imeidhinisha hatua za kusimamisha mauzo ya nje ya gesi, makaa ya mawe na mafuta kutokana na vita vinavyoendelea. Azimio la serikali lililochapishwa Jumatatu lilijumuisha makaa ya mawe, mafuta na gesi inayozalishwa nchini humo, katika orodha ya bidhaa ambazo usafirishaji wake ni marufuku wakati wa vita.