Ukraine: Zelenskiy atembelea vikosi vya msitari wa mbele
6 Juni 2022Mkanda wa vidio uliotolewa na Ikulu ya rais Volodymyr Zelenskiy usiku wa kuamkia leo umemuonyesha rais huyo akizungumza na wanajeshi katika mji wa Lysychansk, na baadaye katika mwingine wa mashariki wa Soledar.
Soma zaidi: Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi
Katika mkanda huo, Zelenskiy anawaambia wanajeshi hao kuwa wanachostahili kukipata ni ushindi, ambao lakini si kwa gharama yoyote.
Tangu nchi yake ilipovamiwa na Urusi tarehe 24 Februari, ni nadra sana rais huyo kutoka katika ngome yake mjini Kiev.
Ziara yawaongezea ari wapiganaji
Baada ya ziara yake katika miji hiyo, Zelenskiy alisema ameshuhudia kwa macho yake madhila yanayowakumba watu wa eneo hilo, na kupongeza ushujaa wao.
''Kwa kila niliyekutana naye, niliyesalimiana naye, niliyezungumza naye, niliona fahari,'' amesema Zelenskiy na kuongeza kuwa ziara yake imewaongezea ari na uthabiti wanajeshi wa Ukraine.
Mji wa Lysychansk uko jirani na ule wa Sievierodonetsk ambao hivi sasa unakabiliwa na mapigano makali.
Soma zaidi: Vita vya Urusi na Ukraine vyaingia siku 100
Taarifa za jana zilieleza kuwa vikosi vya Ukraine vilikuwa vimepata mafanikio, kwa kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi na kuidhibiti nusu ya mji huo muhimu.
Hata hivyo, gavana wa mkoa wa Luhansk ulipo mji huo, Serhiy Gaidai amesema kupitia televisheni ya taifa ya Ukraine kuwa mkondo wa mambo ulibadfilika ghafla na vikosi hivyo vya Ukraine vilikuwa vikijikuta chini ya shinikizo kubwa.
Ingawa hakutoa taarifa za kina, gavana huyo ameongeza kuwa wanajeshi wa Ukraine walikuwa wanasimama kidete kulinda eneo la viwanda katika mji wa Sievierodonetsk, wakati makabiliano makali kuwahi kushuhudiwa katika mji huo yakiendelea.
Urusi kuruhusu usafirishaji wa nafaka
Sambamba na mzozo huo wa vita kati ya Urusi na Ukraine, shirika la habari la Izvestia lenye mafungamano na serikali ya Urusi, limemnukuu afisa wa serikali mjini Moscow aliyesema kuwa Urusi itaruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari ya mji wa Odessa kusini mashariki mwa Ukraine, baada ya makubaliano ya pande tatu, ambazo ni Urusi, Ukraine na Uturuki.
Soma zaidi:Urusi yadhibiti karibu asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine
Hatua hiyo inajiri wakati bei ya bidhaa hiyo ikipanda sana kwenye soko la kimataifa.
Na wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameahirisha ziara aliyotarajiwa kuifanya nchini Serbia, baada ya mataifa jirani na Serbia kuinyima ruhusa ndege yake kupita katika anga yao.
-dpae, afpe, rtre