1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Zelensky awasihi wanajeshi wa Urusi wasipigane

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
1 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika hotuba maalum usiku wa kuamkia Jumapili amewataka wanajeshi wa Urusi, kwa lugha ya Kirusi waache kupigana nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Afg8
Ukraine Krieg I Dobropillya, Donetsk
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Zelensky amesema majeshi ya Urusi yatapata hasara kubwa wakati ambapo yanajiandaa kwa mashambulizi mapya katika eneo la mashariki la Donbas na alitoa wito kwa wanajeshi wa Urusi kuokoa maisha yao, akisema "afadhali kuishi Urusi kuliko kufa kwenye ardhi ya Ukraine."

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Uncredited/Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture-alliance

Rais wa Ukraine pia alizungumzia mashambulio ya anga ya siku ya Jumamosi ambapo uwanja wa ndege katika mji wa pwani wa Odesa uliharibiwa kwa makombora ya Urusi. Odesa ni mji ambao hapo awali ulikuwa kivutio maarufu cha watalii kutoka Urusi.

Gavana wa mkoa wa Odessa, Maxim Marchenko, amesema Urusi imeushambulia kwa makombora na kuuharibu uwanja huo na kuilenga miundombinu na mifumo ya ugavi ya mji huo wa magharibi mwa Ukraine.

Soma:Ukraine yasema huenda mazungumzo ya amani kati yake na Urusi yakasambaratika kabisa

Meya wa mji wa Odesa, Gennadiy Trukhanov, amesema imechukua miaka 10 kuujenga uwanja huo wa ndege, ambao ulifunguliwa rasmi mnamo Julai mwaka jana.

Taarifa zaidi zinafahamisha kuwa takriban raia 20, wakiwemo watoto kadhaa, wamefanikiwa kuondoka kutoka kwenye kiwanda cha chuma kilichopo katika mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine.

Kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa pwani wa Mariupol
Kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa pwani wa MariupolPicha: Musienko Vladislav/Ukrainian News/IMAGO

Kikosi cha jeshi la Ukraine cha Azov, ambacho kimekuwa kikipambana kulikomboa eneo hilo, kimesema raia hao 20 wameondoka, na wameelekea katika mji wa Zaporizhzhia ulio umbali wa kilomita 225 kaskazini magharibi.

Haijafahamika wazi iwapo zoezi hilo la kuwahamisha watu liliongozwa na Umoja wa Mataifa na pia kama shughuli zaidi za kuwahamisha watu zitaendelea.

Soma:UN yaomba amani, Urusi ikiishambulia Ukraine

Hali ni mbaya katika kiwanda cha chuma cha Azovstal ambapo mamia ya raia wanajihifadhi humo ndani pamoja na wanajeshi wa Ukraine. Juhudi za awali za kuwahamisha watu hao ziliambulia patupu.

Wakati huo huo, mwigizaji wa filamu wa Hollywood ambaye pia ni mjumbe maalum na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi, Angelina Jolie, alifanya ziara ya kushtukiza katika mji wa magharibi mwa Ukraine wa Lviv Jumamosi, kwa mujibu wa gavana wa mkoa wa Lviv, Maksym Kozytskyy. Bibi Jolie amekuwa mjumbe maalum wa UNHCR tangu 2011.

Angelina Jolie mwigizaji wa Filamu na mjumbe maalum wa Shirikal la Umoja wa Mataifa la UNHCR.
Angelina Jolie mwigizaji wa Filamu na mjumbe maalum wa Shirikal la Umoja wa Mataifa la UNHCR.Picha: Ospedale Pediatrico Bambino Gesu/AP/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Lviv amesema Angelina Jolie alizungumza na watu walioyakimbia makaazi yao na ambao wamepata hifadhi katika mji huo wa Lviv, wakiwemo watoto ambao wanaendelea kupata matibabu ya majeraha waliyoyapata wakati kituo cha reli cha Kramatorsk kiliposhambuliwa kwa makombora mapema mwezi Aprili.

Vyanzo: AP/RTRE/AFP