1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Ulaya itaepuka hatua za kuzuia COVID-19 kwa mara ya pili?

21 Septemba 2020

Kuanzia katikati mwa miji iliyo mitupu hadi kufungwa kwa biashara, kipindi cha machipuko ambapo shughuli zote za nchi zilifungwa bado kiko kwenye kumbumbuku za watu wengi wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3inhJ
England Leicester Coronavirus Maßnahmen
Picha: picture-alliance/dpa/B. Page

Serikali za Ulaya zina hamu kubwa kuzuia kuweka hatua kama hizo kwa mara nyingine. "Janga", "maafa" na "hali ya kutisha" ni maneno yanayotumiwa na viongozi wa Ulaya kuelezea madhara ya kufungwa kwa shughuli zote za nchi kwa mara ya pili, hatua iliyo wazi zaidi.

Ili kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 wakati wa kipindi cha machipuko mwaka huu, shughuli za umma barani Ulaya zilisimama. 

Wakati wa majira ya joto, maeneo mengi yalilegeza masharti hayo. Hata hivyo, kwa wiki kadhaa sasa viwango vya maambukizi vimekuwa vikiongezeka karibu kwenye kila nchi ya Ulaya.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Ulaya inarekodi kati ya visa vipya 40,000 na 50,000 vya virusi vya corona kila siku. Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Hans Kluge amesema idadi ya kuanzia Septemba inapaswa kuwa kama tahadhari kwa wote. WHO imesema maambukizi ya kila wiki ni mengi kuliko hata yale yaliyorekodiwa mwezi Machi wakati virusi vya corona vilikuwa vimeshika kasi.

Pamoja na ongezeko la maambukizi linakuja suala la kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu kufungwa upya kwa shughulizi za umma nchi nzima. Hatua kali zilizowekwa Uhispania na Ufaransa mwanzoni mwa mwaka huu, zilisababisha mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na sasa idadi ya visa inaongezeka tena kwenye nchi hizo mbili. Hata hivyo, Ufaransa ina matumaini ya kuzuia kuifunga tena nchi hiyo, maadamu inawezekana.

WHO Europa Hans Kluge
Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Hans KlugePicha: Alberto Pizzoli/AFP/Getty Images

Nchi zinaweka vizuizi vya kikanda

Badala yake, maafisa wanaimarisha masharti magumu kwenye miji iliyoathirika vibaya kama vile Paris, Marseille, Bordeaux, Nice na Toulouse. Mikusanyiko imepigwa marufuku, baa zina muda wa saa chache wa kufunguliwa na ziara kwenye nyumba za wazee zimefutwa. Kwa watu wa Paris na maeneo mengine, mtu anapaswa kuvaa barakoa pindi anapoondoka nyumbani kwake. 

Wakati huo huo, Madrid imeanza kuweka vizuizi siku ya Jumatatu. Kwenye wilaya sita na manispaa saba kuzunguka mji huo mkuu wa Uhispania, watu wanaruhusiwa tu kutoka ndani ya nyumba zao kwenda kutafuta huduma muhimu kama vile kwenda kazini, shule, kwa daktari au iwapo umeitwa mahakamani. Hatua kama hizo za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona zimewekwa pia kwenye maeneo mengine ya nchi, ikiwemo Mallorca.

Isabel Ayuso, Rais wa Jimbo la Madrid anasema maeneo ya makaazi yataathiriwa na hatua mpya, iwapo idadi ya maambukizi mapya itazidi 1,000 kwa wakaazi 10,000 zilizorekodiwa siku 14 zilizopita. Ayuso anasema hiyo ilikuwa ni idadi kubwa sana iliyowalazimu maafisa kuchukua hatua na anasema wanataka kuzuia kufungwa kwa nchi nzima, kwani itakuwa wanarudi nyuma na itakuwa janga kwa uchumi wao. 

Madhara ya kiuchumi ya kufungwa kwa nchi nzima kwa mara ya pili huenda yakatanuka zaidi hadi Ulaya Kusini na Magharibi. Nchini Ujerumani, vyama vya wafanyabiashara vinaonya kuhusu wimbi la kufilisika. Mario Ohoven, rais wa shirikisho la viwanda vya kati nchini Ujerumani, anasema moja ya tano ya kampuni zote tayari zimeshuhudia madhara ya mzozo wa virusi vya corona. 

Spahn kündigt neue Corona-Strategie für kalte Jahreszeit an
Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn Picha: Roland Weihrauch/dpa/picture-alliance

Ingawa maambukizi yanaongezeka Ujerumani, kufungwa kwa nchi nzima mara ya pili sio jambo linalofikiriwa. Waziri wa Afya, Jens Spahn anasema kama kila mmoja akichukua jukumu la kujikinga, basi nchi haitofikiria kuzungumzia kuhusu kuweka masharti mapya kuzuia virusi vya corona kusambaa.

Hali ni tofauti nchini Uingereza. Waziri wa Afya, Matt Hancock hivi karibuni alisema wanataka kujizuia na kuifunga tena nchi nzima, lakini pia ametahadharisha wamejiandaa kwa hilo. Takriban watu 42,000 wamekufa kwa COVID-19 nchini Uingereza na hivyo kuifanya kuwa nchi iliyoathirika zaidi barani Ulaya.

Mjini Birmingham, Glasgow na miji mingine mikubwa, watu wa familia moja hawaruhusiwi kukutana na watu wa kaya nyingine kwenye maeneo yaliyofungwa na mikutano kwenye maeneo ya umma pia imezuiwa kwa kiasi fulani.

Ulaya ina hamu ya kuzuia kufungwa tena kwa nchi zake kwa mara ya pili, hatua inayoendelea kwa sasa nchini Israel. Pamoja na kutekeleza hatua katika ngazi ya kitaifa, wanasiasa wanawasihi wananchi kuwa na nidhamu.

(DW https://bit.ly/2FMiD9C)