Ulaya yaimarisha vizuizi vya kukabiliana na corona
28 Machi 2021Ufaransa imekiri kuwa hali ni ''mbaya'' na kuimarisha vikwazo dhidi ya idara tatu zaidi mbali na 16 zilizo chini ya vikwazo hivyo vikali. Watu milioni 20 nchini Ufaransa pamoja na eneo la Paris wameorodheshwa kuishi katika maeneo hatari zaidi kwa maambukizo. Nchini humo, watu hawaruhusiwi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kutoka majumbani mwao bila sababu za kimsingi. Idadi ya kila siku ya maambukizo nchini Ufaransa imekaribia kuongezeka maradufu tangu mwanzoni mwa mwezi Machi na kumekuwa na visa vipya vya zaidi ya elfu 200 kila wiki.
Nchini Uingereza, waziri mkuu Boris Johnson, amesema kuwa kampeni ya serikali ya kutoa chanjo kwa wingi iliyokuwa na tija pamoja na sera zinazonufaisha biashara, kutaharakisha kufufuka kwa uchumi. Wales ni eneo la kwanza la Uingereza kuondoa vikwazo vya usafiri siku ya Jumamosi. Kuanzia siku ya Jumatatu, agizo la kubaki majumabni lililokuwa limetolewa litalegezwa na kuyaruhusu makundi ya hadi watu sita kukutana nje.
Mataifa mengine pia yachukuwa tahadhari dhidi ya virusi vya corona
Wakati huo huo, Ubelgiji ilifunga biashara zote zinazojumuisha mikutano isiyokuwa ya kimatibabu tangu Jumamosi. Maduka yanayotoa huduma zisizouzwa bidhaa za msingi yanaweza tu kupokea wateja kwa miadi.
Poland nayo imeyafunga maeneo ya kuwaangalia watoto kwa muda, viwanja vya michezo na saluni za kike na kiume. Kanuni za kuzingatia umbali kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine pia zimeimarishwa, ambapo mtu mmoja ataruhusiwa kukaa katika kila mita 20 za mraba, badala ya mita 15 za mraba zilizokuwa zimewekwa awali.
Ufilipino ilitangaza Jumamosi kuwa zaidi ya watu milioni 24 ndani na nje ya Manilla wataingia katika vizuizi vikali vya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Msemaji wa rais, Harry Roque amesema kuwa virusi hivyo ni adui na wala sio serikali.
Kuanzia Jumatatu, watu wataanza kufanya kazi majumbani na kuruhusiwa tu kwa wale wanaofanya kazi za huduma za msingi. Usafiri wa umma pia utasimamishwa. Siku ya Ijumaa, Kenya lilikuwa taifa la kwanza barani Afrika kutoa sheria za kufunga baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, shule na baa ndani na nje ya Nairobi. Shirika la Afya Duniani WHO, Ijumaa lilitoa wito kwa mataifa tajiri kutoa msaada wa chanjo kwa mataifa maskini ili yaweze kuanza kampeni zao za chanjo.