Ulaya yaunga mkono makubaliano ya Ukraine
13 Februari 2015Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya waliokutana jana kwenye mkutano wa kilele mjini Brussels wako tayari kuchukua hatua zaidi dhidi ya Urusi ikibidi, kwa lengo la kuishinikiza nchi hiyo kuheshimu makubaliano hayo yaliyofikiwa siku ya Alhamisi (12 Februari) katika mji mkuu wa Belarus, Minsk.
Akizungumza kwenye mkutano wake na waandishi wa habari akiambatana na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine, Rais Tusk alisema njia pekee iliyopo ni kuheshimiwa kikamilifu kwa makubaliano hayo.
"Leo bado tungali na matumaini ya suluhisho la amani lakini kipimo cha kweli kwa hilo ni kuheshimiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Makubaliano ya awali ya Minsk hayakuheshimiwa. Kwa hivyo tunaendelea kuwa na tahadhari hadi maneno yatafisiriwe kuwa vitendo," alisema kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wake, Rais Poroshenko alisema kwamba atajaribu kila awezalo kuyatia vitendoni makubaliano hayo na kuifanya amani ya Ukraine kuwa ndio shabaha kuu, kwani bila ya amani mipango ya ujenzi mpya wa nchi hiyo iliyosambaratishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe haitawezekana.
"Leo Christine Lagarde wa Shirika la Fedha la Kimataifa amezindua programu mpya ya ushirikiano na Ukraine. Hii ni nguzo muhimu sana ya kifedha katika kuleta mageuzini Ukraine. Na ili kuwa na mageuzi yaliyofanikiwa, tunahitaji jambo moja tu, ambalo ni amani. Na kwa hilo, tutafanya kila tuwezalo," aliahidi kiongozi huyo wa Ukraine.
Wasiwasi wa kuvunjwa kwa makubaliano
Mapema Rais Francois Hollande, ambaye pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ndio vinara wa kufikiwa kwa makubaliano hayo, alielezea matumaini yake kwamba sasa Urusi na Ukraine zimepata mahala pa kuanzia kujenga kuaminiana baina yao.
Hata hivyo, naye pia alionya kuwa ghasia zinazoendelea mashariki mwa Ukraine zinaweza kupelekea hasara zaidi kabla ya muda wa mwisho wa kuweka silaha chini hapo usiku wa Jumapili.
Wawili hao, Merkel na Hollande, walifanikiwa kuzipatanisha pande hizo mbili mjini Minsk muda mchache kabla ya kuhudhuria mkutano wa jana wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji.
Katika kuwajulisha viongozi wenzao kile hasa kilichotokea, Kansela Merkel alisema kwamba bado kazi kubwa ingalipo. "Tunajuwa fika kwamba bado kuna mengi yanayopaswa kufanywa, ndio maana tunasema kila jambo linawezekana. Hili likifanikiwa tutaliunga mkono na tutashukuru sana, lakini kama halikufanikiwa hatuondoi uwezekano wa vikwazo zaidi."
Ripoti kutoka mashariki mwa Ukraine zinasema ndani ya kipindi kisichofikia masaa 24 tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo ya Misk, tayari watu 11 wameshauwa, miongoni mwao wanajeshi wanane na raia watatu.
Tangu mzozo huo uanze mwenzi Aprili mwaka jana, watu wapatao 5,500 wameshauawa na 13,000 kujeruhiwa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga