Ulimwengu wamkumbuka Boutros Boutros-Ghali
17 Februari 2016Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilianza kikao chake Jumanne mjini New York kwa dakika moja ya ukimya kumkumbuka Boutros Boutros Ghali, katibu mkuu wa sita wa Umoja huo na mwaafrika wa kwanza kuuongoza Umoja wa mataifa.
Katibu mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemuelezea Boutros Ghali kama mtu aliyeheshimika, aliyebobea katika sheria ya kimataifa, aliyekuwa na uzoefu wa kipekee, elimu na maarifa, katika wadhifa huo wa juu wa Umoja wa Mataifa.
Ban alisema, “kujitolea kwake katika Umoja wa Mataifa, shughuli za umoja huo na watumishi wake, hakukuwa na dosari na kazi aliyoiacha ilikuwa ya kuigwa, akiongeza alikuwa mwanadiplomasia aliyebobea.
Uongozi wa changamoto
Mwanadiplomasia Boutros Boutros Ghali kutoka Misri alikuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1992, lakini kipindi chake kilimalizika ghafla miaka minne baadae, wakati Marekani ilipopinga kwa kutumia kura ya turufu asichaguliwe tena.
Kipindi chake cha Uongozi kilikuwa na changamoto kubwa, kutokana na kushindwa kwa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Rwanda, Yugoslavia ya zamani mgogoro ulioandamana na vita vya Bosnia Herzegovina, Somalia na Mashariki ya kati.
Baada ya kuchukua msimamo tafauti na utawala wa Marekani na mabishano ya mara kadhaa, Marekani ilimgeuka Boutros Ghali na kuamua kumuunga mkono Kofi Annan kutoka Ghana achukuwe nafasi yake mwaka 1996.
Uhusiano na Marekani ulianza kuwa mbaya mwishoni mwa 1993, wakati Marekani ilipoongoza operesheni ya kijeshi nchini Somalia iliosababisha hasara kubwa ya wanajeshi wake.
Matatizo zaidi yalizuka wakati wa operesheni za kusimamia amani katika Yugoslavia ya zamani na baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994, ambayo Umoja wa Mataifa ulishindwa kuyazuwia.
Vikwazo dhidi ya Saddam Hussein
Boutros Ghali aliyalaumu madola makuu. Pia hakukubaliana na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq ambayo wakati huo alikuwa ameivamia Kuwait na kutolewa mwaka mmoja kabla ya Boutros Ghali kuuongoza Umoja wa Mataifa.
Katika kumpinga mwanadiplomasia huyo, aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Madelaine Albright alisema Boutros Ghali ameshindwa kuleta mageuzi yanayohitajika, huku mwenyewe akisema wanaozuwia mageuzi wanafahamika. Baada ya kuondoka Umoja wa Mataifa Boutros Ghali aliteuliwa Katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa – Francophonie.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/afp
Mhariri:Iddi Ssessanga