Umma ndio wenye uwezo wa kuleta utulivu Pakistan
6 Mei 2009Serikali ya Pakistan inapoahidi kuchukua hatua kali, wapiganaji wa Taliban ndio huzidi kusonga bila ya shida na hudhihirisha hali ngumu inayokabiliwa na wanasiasa. Yaonekana kana kwamba hakuna alie na jawabu kuhusu njia ya kupambana na wanamgambo hao - si jeshi la ushawishi mkubwa wala viongozi serikalini au hata raia wenyewe.
Kwani serikali mara hujadiliana nao kama ilivyokuwa katika Bonde la Swat, ambako serikali imekubali kuanza kutumia sheria za Kiislamu na mara huwashambulia kijeshi. Kinachosikitisha ni kuwa mashambulio hayo huchukua maisha ya raia vile vile. Majeshi ya serikali yanashindwa kabisa kuwazuia waasi,lakini viongozi wanakataa kupokea msaada wa Marekani kutoa mafunzo ya kijeshi.Kwani Pakistan kama hapo zamani,inaamini kuwa adui ni India. Na viongozi wa kiraia ndio hushughulikia zaidi mivutano yao wenyewe na kusababisha vurugu.
Kwa upande mwingine wapiganaji wa Taliban waliojiandaa vizuri wanasonga mbele kuteka maeneo yasio na uongozi. Kwa sehemu kubwa wao hutumia vitisho.Kwa mfano katika eneo la Swat na kwengineko, wapinzani ama waliuawa au walifukuzwa makwao kwa nguvu. Wapinzani wa Taliban wanahofia maisha yao.Na idadi ya raia kama hao inazidi kuongozeka kote nchini hasa katika makundi ya walio wachache kama vile Singasinga,Wakristo na hata Waislamu wa madhehebu ya Kishia.
Kiini cha tatizo hilo ni kwamba nchini Pakistan, itikadi kali za kidini na kutovumilia makundi mengine ni kasumba iliyochochewa kwa mpangilio kwa miaka na miaka hasa na wakuu wa kijeshi tangu wakati wa dikteta Zia ul-Haq. Marekani nayo kwa muda mrefu, iliunga mkono na ilishirikiana na wanamgambo kupigana dhidi ya Soviet Union ya zamani nchini Afghanistan.
Sasa kasumba hiyo ndio imebobea na kuwa tatizo kubwa kwa serikali ya Pakistan. Wanamgambo wanaoshambulia majeshi ya NATO nchini Afghanistan au wanaopambana na India huko Kashmir wanaweza kuwa na hakika ya kuuvutia umma nchini Pakistan. Kwani yeyote anaepinga sheria za Kiislamu au asiyekuwa na msimamo wa kidini, hutazamwa kama ni adui wa Uislamu.
Lakini Pakistan,chuki ya nchi za magharibi inahusika zaidi na siasa za serikali ya Bush zilizoaminiwa kuwa dhidi ya Uislamu.Hakuna suluhisho rahisi na hasa si kutoka nje.Marekani imetambua kuwa Pakistan ni muhimu katika ufumbuzi wa tatizo la Afghanistan. Washington inajikuta katika hali ngumu kwani Pakistan ikishinikizwa sana,hatua hiyo huenda ikaongeza wasiwasi na hisia za kutengwa na watakaonufaika ni Wataliban.Kwa kweli ni Pakistan yenyewe itakayoweza kujitoa katika janga hilo.Matumaini pekee ni kuwa sasa, idadi kubwa ya watu nchini Pakistan wametambua hatari inayowakabili na wameanzisha majadiliano, kabla ya maji kufika shingoni.
Mwandishi: T.Bärthlein
Mhariri: Othman Miraji