1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu machafuko Libya

Saleh Mwanamilongo
23 Agosti 2023

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya, Abdoulaye Bathily amezirai pande hasimu nchini humo kumaliza tofauti zao juu ya suala la kufanyika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4VVkq
Libyen | Unruhen in Tripolis
Picha: Yousef Murad/AP/picture alliance

Abdoulaye Bathily ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba migawanyiko ya kisiasa nchini Libya inabeba kitisho cha kutokea machafuko na mparaganyiko kwa taifa kama ilivyoshuhudiwa kwenye mataifa mengine duniani. Mwanadiploamisia huyo ametahadharisha kwamba bila makubaliano jumuishi ya kisiasa yatakayofanikisha uchaguzi huru na wa uwazi, hali nchini Libya itazidi kuzorota.

"Masuala yote yanayohusiana na uchaguzi yanapaswa kutatuliwa kwa majadiliano na maelewano kati ya pande zote husika. Hatua za upande mmoja lazima ziepukwe kwa gharama yoyote ikiwa tunataka kuepusha migogoro mikali kama tulivyoshuhudia katika miaka kumi iliyopita. Mazingira ya uchaguzi yanapaswa kuwa uwanja wa usawa kwa wagombea wote.'', alisema Bathily.

Mgogoro wa hivi sasa wa kisiasa nchini Libya unatokana na kushindwa kuitishwa uchaguzi kama ulivyopangwa tarehe 24 Desemba 2021, na kukataa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah ambaye aliongoza serikali ya mpito mjini Tripoli. Kwa upande wake, Bunge la upinzani mashariki mwa Libya, lilimteua waziri mkuu wake, Fathy Bashagha, lakini alisimamishwa kazi mwezi Mei.

Mapigano mjini kati Tripoli

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Libya, Abdoulaye Bathily
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Libya, Abdoulaye BathilyPicha: DW/C. Wanjohi

Umoja wa Mataifa umesema unafanya kazi na pande zote hasimu ili kuwa na makubaliano ya kina ya kisiasa kuhusu masuala kuhusiana na serikali mpya na kuhakikisha usalama na nafasi kwa wagombea wote katika uchaguzi.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa mataifa kwa Libya,Abdoulaye Bathily aliliambia baraza la usalama kuwa uthabiti tete huko Tripoli ulikuwa umevunjika wiki iliopita kufuatia mapigano makali kati ya wanamgambo hasimu. Machafuko hayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 55 na kujeruhiwa kwa zaidi ya watu mia moja.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield amelaani mapigano hayo kati ya wanamgambo wa Tripoli na kusema ukosefu wa utulivu kwenye nchi jirani ya Sudan na Niger kutasabisha ongezeko la vurugu kubwa zaidi. Huku akisema watu wa Libya wako tayari kwa maelewano na utulivu.

Niger tishio kwa usalama wa kikanda ?

Kuhusu machafuko ya huko Niger, Abdoulaye Bathily amesema kama nchi nyingine ya eneo la Sahel, Niger pia imeathirika na mzozo wa Libya. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya amesema baadhi ya wananchi wa Niger wamejiunga na mamluki nchini Libya. Huku akionya kuwa kuyumbishwa kwa Niger bila shaka kutakuwa na matokeo mabaya kwa Libya.