1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kumchagua mwenyekiti mpya

30 Januari 2017

Viongozi wa Umoja wa Afrika leo kufikia maamuzi magumu juu ya Morocco kujiunga tena na jumuiya hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Kenya apigiwa upatu kuchukua uenyekiti wa AU katika uchaguzi utakao fanyika leo

https://p.dw.com/p/2WcFL
Äthiopien Afrikanische Union Gipfel
Picha: picture-alliance/dpa/K. Tlape

Mkutano huo wa viongozi wa siku mbili unafanyika wakati kuna mtikisiko na mabadiliko katika ngazi za kimataifa kwenye kila pembe ya ulimwengu kuanzia Marekani ambako rais mpya Donald Trump amechukua madaraka baada ya kushinda uchaguzi uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, na kwa upande mwingine Umoja wa mataifa umepata katibu mkuu mpya Antonio Guterres.  Jana Guteress aliisifu Ethiopia kwa ukarimu wake wa kuwakaribisha wakimbizi kutoka kanda hiyo huku yenyewe ikipambana na hali ngumu ya ukame mbaya kuwahi kutokea nchini humo tangu miaka 50 iliyopita.

Bila shaka mazungumzo hayo ya leo ya viongozi wa Umoja wa Afrika yatatawaliwa na swala la Morocco la kutaka kurejea tena katika jumuiya hiyo tangu ilipojitoa kwenye Umoja huo kama ishara ya kupinga hatua ya kutambuliwa kwa Sahara Magharibi kama mwanachama wa Umoja huo miaka 33 iliyopita.

Symbolbild Marokko Afrika-Arabischer Gipfel
Brahim Ghali rais wa Jamuhuri ya Kiarabu ya Sahrawi na katibu mkuu wa PolisarioPicha: Reuters/R. Boudina

Kwa Morocco kurejeshwa katika Umoja wa Afrika itakuwa ni hatua yenye manufaa kwa umoja huo hasa baada ya AU kumpoteza mwanachama muhimu aliyekuwa akitoa mchango mkubwa wa fedha ambaye ni Muammar Gaddaffi wa LIbya.  kwa mujibu wa kituo cha mafunzo ya Usalama cha ISS Umoja wa Afrika unategemea asilimia 70 ya misaada kutoka kwa wafadhili wa nje ili kundesha shughuli zake.  Hata hivyo bado haijafahamika rasmi kama Morrocco itarudishiwa uanachama wake kutokana na nchi zenye nguvu kama Algeria na Afrika Kusini kupinga pendekezo hilo. Nchi hizo mbili zimekuwa zikiunga mkono harakati za kudai uhuru za Sahara Magharibi zinazoendeshwa na kundi la Polisario.  Morocco inashikilia kwamba eneo hilo lililomegwa na Uhispania mnamo mwaka 1975  ni himaya yake. Viongozi hao watazungumzia pia maswala ya usalama, kitisho cha utawala wa Donald Trump na mtazamo wake kwa bara la Afrika, machafuko ya nchini Libya, makundi ya  itikadi kali nchini Mali, Somalia, Nigeria na kuzorota kwa usalama nchini Sudan ya Kusini

Kenia Kabinett 2013 Najib Balala
Amina Mohamed waziri wa mambo ya nje wa KenyaPicha: FABRICE COFFRINI/AFP/Getty Images

Mbali na matukio hayo viongozi wa Umoja wa Afrika wanatarajiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa Umoja huo miezi sita baadae kutokana na kushindwa kumpata mrithi wa Nkosazana Dlamini - Zuma wa Afrika Kusini.  Wakati huu vile vile uchaguzi huo utakuwa mgumu kwa watetezi wa nafasi hiyo kutoka nchi tano za Kenya, Senegal, Chad, Botswana na Guinea ya Ikweta. Mgombea anahitajika kupata theluthi mbili ya kura kuweza kushinda nafasi hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohamed, waziri mkuu wa zamani wa Chad Moussa Faki Mahamat na mwanasiasa mkongwe wa Senegal Abdoulaye Bathily ni wagombea wapya katika kinyag'anyiro hicho.

Mwandishi:  Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu