Umoja wa Afrika umepata kiongozi wa kike
16 Julai 2012Uteuzi huo umemaliza mkwamo katika kinyang'anyiro cha uongozi ambao ulikuwa umetishia kuugawanya na kuudhoofisha Umoja huo. Kulikuwa na shangwe katika makao makuu ya Umoja wa Afrika - AU mjini Addis Ababa, Ethiopia baada ya Nkosazana Dlamini-Zuma ambaye ni mke wa zamani wa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kumshinda kiongozi anayeondoka Jean Ping wa Gabon.
Bibi Zuma alipata uungaji mkono kutoka kwa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, naye Ping akipigiwa upatu na nchi za bara la Afrika zinazotumia lugha ya Kifaransa.
Changamoto zanazomkabili Dlamini-Zuma
Kiongozi huyo mpya anakabiliwa na changamoto nyingi wakati ambapo AU ikijaribu kutafuta uungaji mkono wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuruhusu majeshi kuingia Kaskazini mwa Mali, ambako wanamgambo wametwaa udhibiti wa eneo hilo, baada ya mapinduzi ya jeshi yaliyofanywa katika mji mkuu wa Kusini Bamako.
Uteuzi huo wa waziri huyo wa mambo ya ndani wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 63, ambaye zamani alikuwa waziri wa Afya na Mambo ya Nchi za Kigeni, unamwongezea wasifu wa masuala ya kidiplomasia.
Mgogoro wa Mali, pamoja na mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea-Bissau, na mapigano ya mpakani ya mwezi Aprili baina ya Sudan na Sudan Kusini yamevuruga maendeleo ya bara Afrika katika miaka ya hivi karibuni katika kutafuta uongozi bora na uimara pamoja na ukuaji wa kiuchumi.
Dlamini-Zuma alipitia duru tatu za upigaji kura kabla ya Ping, mwenye umri wa miaka 69 kuondolewa. Duru ya mwisho ya kura 37 ilimpa wingi wa asilimia 60 aliyohitaji kuchaguliwa kwa wadhifa huo.
Kinyang'anyiro kilikuwa kimekwama
Kinyang'anyiro cha kuuongoza Umoja wa Afrika wenye nchi 54, kilikuwa kimekwama tangu uchaguzi wa awali wa mwezi Januari katika mkutano wa kilele kushindwa kumpata mshindi.
Mgogoro huo ulipanuka zaidi katika kikao cha Viongozi wa nchi wanachama wa AU mjini Addis Ababa mwishoni mwa wiki.
Hali hiyo ilimfanya mwenyekiti wa sasa wa AU, Rais wa Benin Boni Yayi kuwaonya Marais wa Afrika ikiwa Umoja huo utashindwa kutatua mkwamo huo wa uongozi, utahujumiwa na kupoteza uhalali wake ulimwenguni.
Ping alikiri kushindwa na akampongeza Dlamini-Zuma kwa ushindi wake. Wahakiki wanasema Umoja wa Afrika ulionyesha kusitasita katika kuikabili mizozo ya mwaka jana nchini Libya na Cote d'Ivoire, na kuzikubalia nchi za Magharibi kuchukua majukumu ya kuongoza.
Katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya kura, Dlamini-Zuma aliondoa hofu kuwa Afruka Kusini huenda ikautumia wadhifa huo wa AU kujaribu kulitawala bara la Afrika. Nchi kadhaa ndogo zilihoji kuwa ugombea wake ulikiuka sheria ambayo haiko katika maandishi kuwa mataifa makuu ya Afrika hayafai kuwania uongozi wa AU.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba